Waziri mkuu wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mizengo Pinda ameungana na makada wengine wa chama cha mapinduzi kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya urais ambapo pamoja na mambo mengine amejinasibu kama atapitishwa atahakikisha anapambana kutekeleza kwa vitendo dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2000-2025 na mpango wa maendeleo wa taifa wa miaka 15.
Pinda ambaye ni miongoni mwa makada waliokuwa wanatajwa katika kinyang'anyiro hicho kwa muda mrefu ametangaza nia na kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo huku kwenye hotuba yake iliyochukua zaidi ya dakika 45 akielezea mikakati mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa dira na mpango wa taifa wa maendeleo ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025.
Katika hotuba hiyo Pinda ameelezea awamu ya kwanza mpango wa taifa ndani ya dira ya maendeleo ya taifa unayomalizika 2016 umejikita katika sekta ya miundombinu na endapo atapewa ridhaa atahakikisha awamu ya pili ya mpango huo inajikita katika mapinduzi ya kilimo na viwanda hususani vya usindikaji mazao na matunda akiwa na imani watanzania wengi watainuka kiuchumi .
Pinda pia akataja maadui wakuu wa tano wa maendeleo ambao amesema ni ujinga, maradhi, umasikini, uharibifu wa mazingira na ukosefu wa utawala bora na akichaguliwa atapambana nao ili kujenga misingi imara ya utawala huku akiapa kula sahani moja na wala rushwa kwa kuifanya taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU kuwa huru bila kuingiliwa katika utendaji wake.
Waziri mkuu huyo akamalizia hotuba yake kwa msemo usemao uchunguzi wa mwana aujuaye mzazi akiwa na maana kuwa yeye ndio msimamizi mkuu wa shughuli za serikali kwa sasa na anatambua changamoto zote zinazowakabili watanzania na anaamini anaweza kukabiliana nazo ili kuboresha maisha ya watanzania katika sekta zote .
