
Lazaro Nyalandu, akizungumza baada ya kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM)
Hayo yamejiri leo jijini Dodoma wakati wa mkutano maalum wa CCM wa kumuidhinisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, huku akitumia nukuu ya biblia kwamba ugenini aliombwa aimbe wimbo sawasawa na Zaburi ya 137:1-4.
"Mh. Mwenyekiti katika nchi ya ugenini wimbo hauiimbiki Mzee Lowassa, Mzee Frederick Sumaye na Mzee Slaa hawa ni mashuhuda wachache kati ya wengi kwanini wimbo wa Bwana hauimbiki katika nchi ya ugenini", amesema Nyalandu.
"Mh. Mwenyekiti Watanzania wameiona nyota yako wameguswa na kujawa na furaha na matumaini tele kwa kuinuliwa kwako, ni maombi yetu kwamba mkono hodari wa Mungu ukakuongoze katika safari iliyotukuka ya kuwaongoza Watanzania", ameongeza Nyalandu.
Mwaka 2017 Lazaro Nyalandu, alitangaza kujivua uanachama ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), na kisha kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambapo alikuwa mtia nia wa kiti cha urais na mgombea ubunge kupitia CHADEMA katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.