DATO SRI IDRIS JALA,MJUMBE MAALUM WA RAIS WA MALAYSIA MHE MOHD NAJIB ALIPOKUTANA NA RAIS MAGUFULI IKULU DAR ES SALAAM.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amemhakikishia Waziri Mkuu wa Malaysia Mhe. Najib Razak kuwa serikali yake ya awamu ya tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na Malaysia hususani katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kukuza biashara na uwekezaji.
Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 24 Juni, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam baada ya kupokea barua yenye ujumbe wa Waziri Mkuu wa Malaysia iliyoletwa kwake na Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu huyo Mhe. Dato Sri Idris Jala ambaye ni Waziri katika ofisi ya Waziri Mkuu wa Malaysia.
Pamoja na kupokea barua hiyo, Rais Magufuli na Mhe. Dato Sri Idris Jala wamezungumzia miradi mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Malaysia, na wametilia mkazo umuhimu wa kuitumia vizuri sekta binafsi katika uwekezaji kwenye miradi ya maendeleo hususani viwanda, miundombinu na maendeleo ya makazi.
"Naomba unifikishie shukrani zangu za dhati kwa Waziri Mkuu wa Malaysia Mhe. Najib Razak na umwambie kuwa serikali yangu itaendelea na kukuza zaidi ushirikiano na Malaysia na nitafurahi zaidi kama mahusiano na ushirikiano wetu utajikita katika kubadilishana uzoefu juu ya kupata mageuzi katika uchumi kama ambavyo Malaysia imefanya.
"Nawakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Malaysia na kwa kuwa nchi yenu ina shirika kubwa la ndege basi itakuwa ni vyema kama uzoefu mlionao tukashirikiana kwa kuwa nasi tumeamua kufufua shirika letu la ndege na kwa kuanzia tutanunua ndege tatu hivi karibuni" Amesema Rais Magufuli.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na Balozi wa Norway hapa nchini Mhe. Hanne-Marie Kaarstand ambapo pamoja kuzungumzia uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili katika masuala mbalimbali yakiwemo uwekezaji katika sekta ya nishati na kilimo, wamezungumzia kuendeleza ushirikiano huo katika mapambano dhidi ya rushwa na ujangili kwa kuimarisha vyombo vinavyohusika ambavyo ni Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), Mahakama na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP).
Kwa upande wake Balozi wa Norway hapa nchini Mhe. Hanne-Marie Kaarstand amesema tangu miaka ya 60 mpaka sasa Norway imetumia dola za kimarekani Bilioni 2 kuunga mkono miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za kijamii kwa Tanzania na kwamba itaendelea kushirikiana na Tanzania kama ambavyo hivi sasa inafanya kazi na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) katika kudhibiti matumizi na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Finland hapa nchini Mhe. Pekka Hukka ambapo Balozi huyo amesema Finland inatambua na inaunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli katika kuhimiza uchapa kazi, ulipaji wa kodi na kukabiliana na rushwa.
Mhe. Pekka Hukka pia amemhakikishia Dkt. Magufuli kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya maendeleo yakiwemo kuwajengea uwezo viongozi, utunzaji wa misitu na hifadhi za wanyama pamoja na maendeleo ya elimu.
Kwa upande wake Rais Magufuli amemuomba Balozi huyo kufikisha shukrani zake kwa Rais wa Finland Mhe. Sauli Niinisto na kumweleza kuwa serikali yake ya awamu ya tano itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano na Finland, na ameiomba nchi hiyo kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha vyombo vya kupambana na rushwa ambavyo ni TAKUKURU, Mahakama na Ofisi ya DPP.