Aliyekuwa Mbunge wa Babati Mjini (CHADEMA), Pauline Gekul.
Akizungumza na www.eatv.tv, Gekul ameeleza kuwa amefanya hivyo ili kutimiza wajibu kwa wananchi wake kwani anashindwa kuzitimiza ahadi hizo akiwa upande wa upinzani.
Gekul amezungumzia suala la kuwa huenda amelipwa pesa ili kujiunga na CCM, ambapo amesema kuwa "Sijanunuliwa na nina kwenda CCM nikiwa siwafahamu kabisa lakini nashukuru nimepata mapokezi mazuri na nitakwenda kuwajua huko huko, wala sijanunuliwa kama wanavyosema".
Gekul amesema kuwa amechoshwa na matabaka yaliyomo ndani ya CHADEMA, kutokusikilizwa na kuthaminiwa kwa baadhi ya watu na wengine akidai kuwa wanaonekana kama chaguo la tatu mbele ya viongozi.
Barua ya kujizulu kwa Gekul ilianza kusambaa kwa kasi mitandaoni jana, Oktoba 13, saa 4 usiku kwenda kwa Spika wa Bunge Job Ndugai, ambapo sasa anaungana na wengine waliojizulu hivi karibuni akiwemo, Mwarya Chacha (Serengeti) na James Milly wa Simanjiro, wote wa CHADEMA.
Gekul anakuwa Mbunge wa nane kujiuzulu kutoka upinzani kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) na kupewa nafasi ya kugombea tena nafasi hiyo, wabunge hao ni; Dkt. Godwin Mollel (Siha-CHADEMA) na Maulid Mtulia (Kinondoni-CUF) huku wanaosubiri kuapishwa ni, Mwita Waitara (Ukonga), Julius Kalanga (Monduli) na Zuberi Kuchauka (Liwale-CUF) ambaye aliibuka mshindi katika uchaguzi uliofanyika jana Jumamosi Oktoba 13,2018 kwa ushindi wa asilimia 85.