Jumanne , 25th Feb , 2025

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya ziara ya kikazi katika maeneo ya Bumbuli, Lushoto, Mkomazi, na Korogwe, akilenga kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza changamoto za wananchi.

Wananchi katika mikutano ya Rais Samia

Katika ziara hizo, amesisitiza umuhimu wa mshikamano kati ya serikali na wananchi katika kutekeleza miradi inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania. Aidha, aliwataka viongozi wa maeneo husika kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kwa viwango vya juu vinavyostahili.  

Akiwa Korogwe, Rais Dkt. Samia aliweka jiwe la msingi katika ujenzi wa bwawa la Mkomazi pamoja na kushuhudia utiaji saini wa mikataba miwili ya ujenzi wa skimu za umwagiliaji za Mkomazi na Chekechea wilayani Korogwe, mkoani Tanga.

Mradi wa Mkomazi, wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 18, unatarajiwa kuhudumia vijiji 28 katika kata saba za Wilaya ya Korogwe, huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 2025.  

Katika wilaya ya Bumbuli, Rais Dkt. Samia alizindua jengo la Halmashauri ya wilaya ya Bumbuli, hatua inayolenga kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi wa eneo hilo.  

Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya mkoa wa Tanga. Kuanzia mwaka 2021 hadi mwanzoni mwa mwaka huu, serikali imepeleka takribani shilingi trilioni 3.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, huku sekta ya afya pekee ikipokea shilingi bilioni 65.6 ili kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa mkoa huo.