Kafulila ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na EATV baada ya mahakama kuu kanda ya Tabora kupitia kwa Jaji Sam Rumanyika Januari 14, 2016 kutupilia mbali mapingamizi ya wakili wa serikali yaliyowasilishwa na kujadiliwa katika mahakama hiyo.
''Nina imani na mahakama na si Majaji wote hawatendi haki nina ushahidi wa kutosha wa fomu namba 21B kutoka vituoni 382 ambazo zilisainiwa na mawakala zikionesha wazi kwamba mimi ndiye mshindi wa halali wa jimbo langu hivyo mkurugenzi wa halmashauri ya Uvinza alikosea tu kutangaza mshindi na akamtangaza mwingine lakini mimi ndiye mshindi'' Amesisitiza Kafulila.
Aidha amesisitiza kuwa hawezi kusubiri hadi mwaka 2020 wananchi waongozwe na mtu ambaye hakupewa ridhaa ya wananchi na litakuwa ni jambo la ajabu kufanya hivyo.
Pia Jaji mkuu ametoa siku 90 ili kesi zinazohusu uchaguzi ziweze kukamilika hivyo nina imani kwamba kabla ya mwezi wa tatu maamuzi yatakuwa yamekwisha toka na ukweli kujulikana.
Kuhusu namna ambavyo amewatumikia wananchi wa jimbo lake Kafulila amesema kwamba yeye ni mbunge ambaye amefanya kazi kubwa ya maendeleo kuliko wabunge wote ambao wamepita katika jimbo lake.
''Nimefanya mambo 35 katika jimbo langu ,nimesomesha wanafunzi 200, nimenunua vitanda na magodoro katika zahanati mbalimbali, nimewezesha mawasiliano ya simu kusikika kwa urahisi katika ukanda wa Kigoma kusini, mimi ni mbunge pekee katika jimbo la Kigoma ambaye nilipeleka vifaa vya maabara katika shule zote za kata kabla hata ya mpango wa serikali'' Amesema Kafulila.
Hata hivyo Kafulila amekataa vikali kutikiswa na ngome ya Chama cha ACT Wazalendo katika ukanda wake na kusema kuwa ACT haina ngome kwani ina Mbunge mmoja tu bora NCCR ambayo iliweza kusimamisha wabunge 4 kuliko chama hicho ambacho kimeambulia mbunge mmoja pekee