Jumapili , 18th Aug , 2024

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imesema kuwa shughuli za utalii katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro zinaendelea vizuri pamoja na uwepo wa baadhi ya wananchi wanaoishi katika hifadhi hiyo kuandamana hii leo Agosti 18, 2024.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Meneja, Kitengo cha Uhusiano kwa Umma wa Mamlaka hiyo Hamis Dambaya, imesema kuwa watalii kutoka ndani na nje ya nchi wameendelea na safari zao za kushuhudia vivutio vya utalii ndani ya hifadhi na serikali inaendelea kuwahakikishia usalama wao.

"Maandamano yaliyoripotiwa kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii yanaidhihirishia dunia na jumuiya za kimataifa, vyombo vya habari na asasi za kimataifa kwamba ndani ya Hifadhi hiyo hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa wananchi, Mamlaka inawahakikishia watalii wote waliopanga safari za kuja Ngorongoro kuwa serikali itaendelea kusimamia usalama wao wakati wote watakapokuwa ndani ya hifadhi," imeeleza taarifa hiyo.