Tume ya taifa ya uchaguzi NEC imekanusha taarifa kuwa kuna uwezekano wa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani kuahirishwa kutokana na uwezekano wa kutokamilika kwa daftari la kudumu la wapiga kura.
Aidha NEC pia kupitia kwa mwenyekiti wake Jaji mstaafu wa mahakama ya rufaa Damian Lubuva imesema imepokea BVR 248 na kufanya jumla ya mashine hizo kufikia 498.
Jaji Lubuva amesema baadaye leo wanatarajia kipokea BVR 1600 zitakazowasili kwa ndege ya kukodi ambayo imeshaondoka Dubai kuja jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti huyo wa tume ya taifa ya uchaguzi ametaja awamu ya pili ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura itaendelea April 24 mwaka huu, siku ambayo pia watapokea BVR nyingine 1600 ambazo amesema zitaharakisha kasi ya uandikishaji.
Awamu ya pili ya zoezi la BVR itakuwa katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa.
Kauli ya Jaji Lubuva imekuja siku moja baada ya mwenyekiti wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendelea CHADEMA Freeman Mbowe kuitahadharisha serikali iachane na mpango wowote wa kuahirisha uchaguzi mkuu wa Oktoba kwa kigezo cha kutokamilika kwa daftati la kudumu la wapiga kura.