Jumatatu , 5th Oct , 2015

Makamu mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Severina Mwijage, amewataka wananchi kuwapiga vita na kuto wathamini mabalozi na wenyeviti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwasababu hawatambuliki kikatiba.

Makamu mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Severina Mwijage

Akizungumza jana mkoani Mtwara katika mikutano yake ya kunadi sera za chama na kuwaombea kura wabunge na madiwani wa halmashauri ya Mtwara vijijini, amesema viongozi hao wamewekwa kwa ajili ya kuuhujumu upinzani na kwamba mwisho wao ni mwezi Oktoba mwaka huu.

Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 25 kwa ajili ya kupigia kura UKAWA na kutokuwa na wasiwasi wowote juu ya kuibiwa kura na kwamba uwezekano huo haupo kutokana na kuwepo kwa viongozi mbalimbali ambao awali walikuwepo CCM kabla ya kuingia upinzani.

Akizungumzia namna watakavyoweza kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa halmashauri ya Mtwara vijijini ambazo ni pamoja na elimu, maji na afya, alisema jambo la kwanza ni kufumua mikataba ya rasilimali za gesi asilia na mafuta ambayo wanaamini ndio imebeba utajiri wa wananchi wa maeneo hayo na Kusini kwa ujumla.