Alhamisi , 19th Feb , 2015

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Shamariwa A kata ya Igoma wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, Julius Makoye (CCM), amekutwa amejinyonga juu ya mti ulio jirani na nyumba yake.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Japhet Lusingu.

Makoye alishinda kiti hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba 14 mwaka jana, akiwa ameongoza mtaa huo kwa awamu ya pili baada ya kuongoza miaka mitano iliyopita.

Mke wa marehemu, Ivona Polikalapo, amesema juzi saa 10 jioni alimsikia mumewe akiongea na mtu kwenye simu yake ya mkononi na kumsisitiza anahitaji mzigo wake wote.

Amesema ilipofika saa 10 alfajiri jana, mbwa wao walisikika wakibweka kwa muda mrefu hali iliyomfanya marehemu atoke nje kuangalia kilichopo katika banda lao la mifugo huku (mke) akiendelea kuandaa chakula cha mifugo.

Mama huyo anasema baada ya muda alitoka nje kwenda kumwaga uchafu shimoni, lakini alishangazwa kumuona ananing’inia juu ya mti na alipojaribu kumuita hakuweza kuitika.

Hata hivyo, kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Japhet Lusingu, amethibitisha kuwapo na tukio hilo na kusema amejinyonga huku chanzo chake hakijafahamika.