Jumamosi , 25th Apr , 2015

Mwanamke mmoja mkazi wa Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma amelazwa katika hospitali ya Rufaa mkoani huo baada ya Kufinywa na kuchapwa na muuguzi katika kutuo alichokwenda kujifungulia.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt, Seif Rashid,

Mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Mariamu Maroda mkazi wa kijiji cha Muungano wilayani Chamwino amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) baada ya kufanyiwa ukatili huo katika kituo cha afya cha Muungano alipokwenda kwa ajili ya kujifungua.

Mwanamke huyo amelazwa katika chumba hicho tangu April 3 mwaka huu siku ambayo ilikuwa ni Ijumaa kuu kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma, ndugu wa mgonjwa huyo wamemtuhumu muuguzi wa Zahanati ya Muungano iliyopo katika Kijiji cha Muungano wilayani Chamwino (ambaye hawakumtaja jina lake) kwa kumchapa viboko mama huyo wakati akijifungua hali iliyosababisha kupoteza mtoto.

Mama mdogo wa mama huyo Joyce Charles amesema kuwa muuguzi huyo alimchampa ndugu yao viboko katika sehemu mbalimbali za mwili wakati alipoenda zahanati hapo wakati wa kujifungua.

Kwa upande wake muuguzi mkuu wa hospitali ya mkoa wa Dodoma, Anatoria Mkindo amekiri kuwepo kwa mgonjwa huyo na kwamba kutokana na taarifa za mgonjwa huyo waliagiza ofisi ya mganga mkuu wa wilaya hiyo kupeleka taarifa kwa mganga mkuu wa mkoa kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi ya nesi aliyefanya kitendo hicho.

Naye afisa muuguzi anayemuhudumia katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) Christina Mlumba amesema mgonjwa huyo alipelekwa baada ya kufanyiwa oparesheni na hali yake kwa sasa inaridhisha tofauti na alivyopelekwa.

Kwa upande wa jeshi la polisi kamanda wa polisi mkoa David misime amesema hana taarifa juu ya tukio hilo na kuahidi kulifuatilia.