Alhamisi , 30th Aug , 2018

Mkuu wa majeshi mstaafu nchini, Jenerali Davis Mwamunyange ameteuliwa na Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa kuwa mjumbe wa tume ya watu saba itakayochunguza vurugu zilizojitokeza baada ya uchaguzi nchini humo kabla ya kuapishwa kwake.

Mkuu wa majeshi mstaafu nchini, Jenerali Davis Mwamunyange.

Tume hiyo inatarajiwa kuchunguza kiini cha vurugu hizo ambazo zilisababisha  vifo vya watu sita baada ya wanajeshi kuzima maandammano ya wapinzani siku mbili baada ya uchaguzi wa Julai 30.

Uchaguzi huo ambao umehalalisha urais wa Mngangagwa ulitazamiwa kuwa ni mwanzo mpya wa siasa za kidemokrasia tangu kung'olewa madarakani kwa Robert Mugabe Novemba 2017.

Jenerali Mwamunyange ambaye alikuwa mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa miaka 10 toka 2007 mpaka alipostaafu 2017 ndio mtu pekee katika tume hiyo mwenye uzoefu na jeshi huku wengine wakiwa na taaluma tofauti.

Wengine watakaounda tume hiyo ni mwanasheria kutoka Uingereza Rodney Dixon ambaye aliiwakilisha serikali ya Kenya katika kesi ya vurugu za baada ya uchaguzi wa 2007 katika mahakama ya ICC, The Heague pamoja na katibu mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Madola Chifu Emeka Anyaoku kutoka Nigeria.

Kutoka Zimbabwe wajumbe ni Profesa Charity Manyeruke na Profesa Lovemore Madhuku kutoka chuo kikuu cha Zimbabwe pamoja na Vimbai Nyemba ambaye ni rais wa zamani wa chama cha wanasheria wa Zimbabwe. Huku Rais mstaafu wa Afrika Kusini Bw. Kgalema Motlanthe ataongoza tume hiyo ambayo inatarajiwa kumaliza kazi yake ndani ya miezi mitatu.