Ijumaa , 31st Mei , 2024

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema mei 29, 2024 muda wa saa 08:22 mchana huko katika maeneo ya Elerai Jijini Arusha walifanikiwa kumkamata Peter Mwacha (18) dereva bajaji na mkazi wa Sombetini Jijini Arusha akiwa anasafirisha  dawa za kulevya pamoja na mtuhuiwa wa maujaji.

Bajaji iliyotumika kubeba dawa za kulevya

Akitoa taarifa hiyo leo Kamanda wa Polisi Mkao wa Arusha Kamishna Msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na dawa hizo bunda 316 zenye uzito  wa kilogramu 98.55.

Ameongeza kuwa mtuhumiwa huyo anasafirisha dawa hizo kwa kutumia bajaji yenye namba za usajili MC 541 CXL aina ya TVS huku akibainisha kuwa taratibu zingine za Jeshi hilo zinakamilishwa ili mtuhumiwa afikishwe katika vyombo vya sheria.

Kamanda Masejo amesema katika tukio jingine Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa mauaji Ramadhan Yahaya 28 maarufu kwa jina la Msambaa ambaye alihusika katika tukio la mauaji yaliyofanyika mei mwaka huu eneo la Daraja mbili Jijini Arusha.

SACP Masejo amebainisha kuwa hali ya jiji la Arusha ni shwari ingawa yapo matukio madogo madogo ambayo wahalifu waliotenda uhalifu huo wanaendelea kukamatwa kama alivyokamatwa mtuhumiwa huyo aliyekimbilia jijini Dodoma baada ya kutenda tukio hilo.

Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi Mkoani humo kwa kutoa taarifa za kweli za kihalifu kwenye vyombo vya dola au Serikali za mitaa huku akiwataka kutokutoa taarifa kwenye mitandao zisizo za kweli  ambapo amesema inasababisha wahalifu kukimbia na kukwepa mkono wa sheria ikiwa ni Pamoja na kuleta taharuki na hofu kwa Wakazi na wageni wanaotembelea Mkoa huo.