Jumatatu , 19th Mei , 2014

Mtoto mmoja Wilayani Korogwe amegundulika amefungiwa ndani ya Chumba kwa muda wa miaka 9 kutokana na hali yake ya ulemavu.

Mtoto aliyekuwa amefungiwa kama alivyokutwa na kamera ya EATV

Mtoto mwenye ulemavu wa akili mwenye umri wa miaka 15 amefungiwa chumbani na mama yake wa kambo kwa muda wa miaka 9 ambapo amekuwa akijisaidia humo choo kikubwa na kidogo kisha kuwekewa chakula katika bakuli lake maalum ndani ya chumba hicho hatua ambayo inaweza kumsababishia magonjwa.

EATV imeshuhudia mtoto huyo akiwa chumbani na upande mmoja wa kanga huku kukiwa na vinyesi na bakuli lake analowekewa chakula mithili ya mnyama.

Mtoto huyo alipoona wadau wa dawati la jinsia wa jeshi la polisi wilayani Korogwe wameingia ndani ya chumba hicho pamoja na akina mama wa asasi inayojihusisha na utetezi wa haki za watoto nchini ya ''Pamoja Tuwalee'' aliruka juu kwa furaha ya kuangalia nje huku akiwakumbatia akina mama waliokwenda kumtoa chumbani kwa furaha hatua ambayo ililalamikiwa vikali na wadau hao kwa kufanyiwa vitendo vya kikatili vya aina hiyo.

Mama mlezi wa mtoto huyo mlemavu aliyejulikana kwa jina la Hadija Makame alipoulizwa kuhusu kitendo cha kumfungia ndani mtoto huyo mlemavu ambaye ana uwezo wa kujitambua lakini ameathirika zaidi kisaikolojia baada ya kufichwa ndani kwa muda mrefu amesema kuwa huwa anamtoa nje kwa chakula na hata kumsindikiza chooni majibu ambayo wadau hao walipingana naye baada ya kushuhudia ndani ya chumba chake kukiwa na vinyesi na bakuli lake la kulia chakula.

Kufuatia hatua hiyo shirika la kimataifa linalojihusisha na utetezi na usimamizi wa haki za watoto la ''Pamoja Tuwalee'' inayofadhiliwa na shirika la misaada la watu wa marekani (USAID) inayoshirikiana na serikali  imelalamikia kitendo hicho kwa sababu haki ya elimu kwa watoto walemavu lazima ipewe kipaumbele na ndiyo maana wamezindua vilabu vya kutetea haki za watoto na kufahamu wajibu wao vipatavyo 11 wilayani Korogwe ili kuhakikisha kuwa haki za watoto hasa katika sekta ya elimu na afya inazingatiwa.