
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Oktoba 8,2023 imesema Tanzania inalaani ukatili uliotokea na kusema vurugu hazijawahi kuwa njia bora ya kutatua matatizo huku ikitoa wito kwa pande zote kutafuata amani ya kudumu kwa njia ya kukaa mezani na kufanya mazungumzo ili kuepusha vifo na majanga zaidi.
Taarifa ya msimamo wa Tanzania unaendeleza taarifa za taasisi na jumuiya nyingine za Kikanda ikiwamo Umoja wa Afrika ambao umeeleza kusikitishwa na vita hiyo ambapo imetoa wito kwa pande zote mbili kukomesha mara moja uhasama wa kijeshi na kurudi kwenye meza ya mazungumzo bila masharti na kutekeleza mpango wa kuunda Nchi mbili.
Mwenyekiti wa AU Moussa Faki Mahamat amesema mzozo huo utakuwa na athari mbaya kwa maisha Watu ambapo amesema sababu ya vita hiyo ni kukataliwa kwa haki za kimsingi za Watu wa Palestina hususani ile ya kuwa na Serikali huru.
Siku ya Jumamosi Hamas ilitekeleza shambulio la kushtukiza ambalo lilishirikisha Wapiganaji kadhaa walioingia katika miji ya Israeli karibu na ukanda wa Gaza na baadaye kukafutiwa na mashambulizi makali ya roketi na vurugu baina ya pande mbili ambayo bado yanaendelea kutekelezwa.
Kufuatia hali hiyo baraza la mawaziri la usalama la Israel limetangaza rasmi hali ya vita, kulingana na ofisi ya vyombo vya habari vya serikali Jumapili huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiapa nchi hiyo kulipiza kisasi kikubwa kwa shambulio la wanamgambo wa Kipalestina.
Idara ya habari ya Israel imesema tamko la vita lilichukuliwa kwa mujibu wa Kifungu cha 40 cha Sheria ya Msingi ya Israeli hata hivyo Israeli haina katiba iliyoandikwa lakini Sheria zake 13 za Msingi zinafanya kazi sawa.
Afisa mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Israel anayesimamia shughuli katika maeneo ya Palestina alisema baada ya mashambulizi hayo kwamba Hamas "imefungua milango ya kuzimu." Israel imekuwa ikiishambulia Gaza kwa mashambulizi ya anga ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 300.