Alhamisi , 8th Jul , 2021

Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amewataka wananchi kufuata sheria na taratibu za ardhi na mipango miji pindi wanapotaka kujenga ili kujiepusha na hasara zinazoweza kujitokeza ikiwemo kuvunjiwa nyumba zao.

Pichani Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula

Dkt. Mabula amesema hayo akizungumza na wananchi wa kata za Kahama na Kiseke ikiwa ni muendelezo wa ziara yake, ambapo aliwataka wananchi kuhakikisha kabla ya kununua eneo na kulifanyia maendeleo kujiridhisha na matumizi sahihi ya ardhi ya eneo hilo kwa kushirikisha ofisi za ardhi za majiji na Manispaa za eneo husika ili kupunguza migogoro na kuingia hasara.

“Ni marufuku kujenga kiholela katika maeneo yote ya Manispaa kwa sababu yalishatangazwa kama maeneo ya miji, huwezi kufanya uendelezaji wowote bila kuwa na kibali, bila kuwa na ramani, bila kuhusisha ofisi zinazohusika,” amesema Dkt. Mabula.

Sambamba na hilo Dkt. Mabula amewataka wananchi kuacha kununua ardhi kiholela kwani kila kipande cha ardhi kimepangiwa matumizi yake.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Afisa Ardhi na Mipango Miji Shukran Kyando amekemea vitendo vya matumizi ya ardhi bila vibali vya Manispaa ikiwemo kuendesha biashara ya ufyatuaji wa matofali katikati ya makazi ya watu jambo linalochangia uharibifu wa mazingira kwa kuzalisha kelele.