
Marehemu Juliana Issa enzi za uhai wake
Msanii huyo anafanya shughuli zake ndani ya Kituo cha Utamaduni kilichopo Chuo Kikuu cha Makumira Wilayani Arumeru Mkoani Arusha
Aidha mwili huo wa Juliana ulikutwa mtupu na pembeni yake kulikuwa na nguo zake ambapo uchunguzi wa awali umebaini kuwa mwili wake umekutwa na alama za kucha shingoni na uvimbe sehemu za siri.
Baadhi ya mazingira katika chuo hicho
Akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake Jijini Arusha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema tukio hilo lilitokea jana saa 11:30 asubuhi eneo la Makumira.
Alisema taarifa za awali zinaeleza kuwa Novemba 1 mwaka huu muda wa saa 18:30 jioni marehemu aliondoka nyumbani kwake kwenda kwenye sherehe ya kuzaliwa "Birthday Party" ya rafiki yake ambayo ilipangwa kufanyika kwenye baa iitwayo V. I. C iliyopo eneo la Kilala lakini hakuonekana katika sherehe hiyo.
Baadhi ya wasanii katika kituo hicho
Siku ya pili Novemba 2, polisi walipata taarifa juu ya kuwepo kwa mwili ambao umekutwa kando ya barabara ya kuelekea Ndolo Lodge, baada ya askari kufika eneo hilo walikuta mwili huo ukiwa mtupu na pembeni yake kulikuwa na nguo zake.
Alisema uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa mwili huo ulikutwa na alama za kucha shingoni na uvimbe sehemu za siri kitendo kinachoashiria alikuwa amebakwa.
Alisema hadi sasa chanzo cha kifo hicho bado hakijajulikana na hakuna mtuhumiwa yeyote aliyekamatwa huku msako ukiwa unaendelea ili kuwabaini wahusika wa tukio hilo huku mwili wake ukiwa umehifadhiwa hospitali ya Mount Meru kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi wa daktari.
Awali EATV ilifika kituo cha Utamaduni kilichopo Chuo kikuu cha Tumaini Makumira Wilayani Arumeru kwaajili ya kujua kama Juliana alikuwa ni mwanafunzi wa chuo hicho au la na kuzungumza na Mratibu wa Kituo hicho cha Sanaa (CAC), Randy Stubbs ambaye alisema kuwa hakuwa mwanafunzi bali msanii wa kikundi cha sanaa chuoni hapo.
Stubbs alisema amehuzunika na kifo cha msanii huyo ambaye yeye ni kama mwanaye aliyemuasili.
Alisema jana alimuomba ruhusa kuwa anakwenda kwenye sherehe ya kuzaliwa ya rafiki yake ambaye hakumtaja jina lakini hakurudi nyumbani na kila akimpigia simu haipokelewi na kwamba baadaye haikuita kabisa.
Alisema walihangaika pamoja na wasanii wenzake zaidi ya 25 wa kituo hicho kumtafuta bila mafanikio na jana majira ya saa 11:30 asubuhi walipata taarifa kuwa mwili huo umepatikana maeneo hayo.
