Jumanne , 2nd Sep , 2014

Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali nchini Tanzania inakabiliwa na uhaba wa vifaa kwa ajili ya kupima sampuli zinazohisiwa kuwa za dawa za kulevya kwani vifaa vilivyopo sasa ni vikuu na vimepitwa na wakati.

Mkemia Mkuu wa Serikali nchini Tanzania, Profesa Samwel Manyelle.

Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi ya Makosa ya Jinai na Vinasaba wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Bi. Gloria Omar, amesema hayo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Bi. Gloria amesema vifaa vilivyopo sasa haviwezi kupima sampuli kulingana na mabadiliko ya wahalifu hususani wanaovusha dawa za kulevya kwa kutumia mbinu za kisasa, zikiwemo zile za kuchanganya dawa hizo na vitu vingine kiasi cha kufanya isiwe rahisi kuonekana katika mashine za kawaida.

Wakati huo huo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imesema kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na baadhi ya idara na taasisi za serikali ikiwemo jeshi la polisi.

Mkurugenzi wa Hudama za Kisheria wa Tume hiyo Bw. Nabory Assey amesema hayo na kutaja baadhi ya makosa ya ukiukwaji wa haki za binadamu kuwa ni utesaji, kuuwawa kwa mahabusu pamoja na watu kubambikiwa kesi.

Kwa mujibu wa Bw. Assey, hatua kadhaa zimechukuliwa na tume hiyo kuhakikisha kuwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinapungua, ikiwa ni pamoja na kutoe elimu ya haki za binadamu kwa askari na maofisa wa polisi, hasa vipengele vinavyohusu haki za watuhumiwa na uzingatiaji wa haki za binadamu wakati wa upelelezi.