Jumanne , 28th Jul , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli amemuelezea rais wa Tanzania wa awamu ya tatu hayati Benjamin William Mkapa kama baba wa Demokrasia nchini kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa tangu nchi ilipoingia katika mfumo wa vyama vingi.

Rais Dkt John Magufuli akitoa hotuba Uwanja wa Uhuru wakati wa zoezi la kitaifa la kutoa heshima za mwisho kwa miwili wa hayati Benjamin Mkapa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli amemuelezea rais wa Tanzania wa awamu ya tatu hayati Benjamin William Mkapa kama baba wa Demokrasia nchini kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa tangu nchi ilipoingia katika mfumo wa vyama vingi.

Rais Dk. Magufuli ametoa kauli hiyo leo katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam wakati wa zoezi la kitaifa la kutoa heshima za mwisho kwa miwili wa hayati Mkapa, ambapo amesema msiba wa Mzee Mkapa sio msiba wa familia yake tu bali ni msiba wa taifa zima.

Amesema kuwa katika kipindi chake chote Mzee Mkapa ambaye alikuwa rais wa kwanza aliyechaguliwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1995, baada ya kurudishwa kwa mfumo huo mwaka 1992, alikuwa akijitahidi kujenga Demokrasai nchini.

Pia amesema Mzee Mkapa atakumbukwa kwa mageuzi makubwa ya kiuchumi aliyoyafanya kwa kulipa madeni na kutumia uzoefu wake wa kidiplomasia kurejesha uhusiana na taasisi za kifedha za kimataifa na nchi wahisani, na kufanikisha nchi kusamehewa deni la dola za Marekani bilioni 3 kati ya dola za Marekani bilioni 7 kupitia mpango wa msamaha wa madeni wa HPIC.

Katika kuonyesha Mzee Mkapa alikuwa anawajali wananchi wanyonge, rais Dk. Magufuli amesema Mzee Mkapa alifuta kodi ya kichwa ambayo ilikuwa ikileta usumbufu sana kwa wananchi pamoja na kufuta kodi ya baiskeli na kodi ya mifugo.

Akiongea kwa huzuni kubwa Rais Dk. Magufuli amesema kwamba Mzee Mkapa amemtendea mambo mengi mema na kuongeza kwamba wakati wote alikuwa anamchukulia Rais Magufuli kama mtoto wake na alikuwa akimlea kwa upendo.

“Mzee Mkapa alikuwa na vipaji vya kulea na kukuza, yeye ndiye aliniibua mimi, alimteua Mzee Kikwete kuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa miaka 10 baadaye akawa mrithi wake ni kama alikuwa anamuandaa kuwa Rais, alimuibua Rais Shein kwa kumpa Umakamu wa Rais”

Awali Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi alisoma wasifu wa hayati Benjamin William Mkapa.

Zoezi la heshima za mwisho lilihudhuriwa na marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wa Burundi Mhe. Jenerali Alain Guilaume Mwili wa rais mstaafu wa awamu ya tatu umewasili Wilayani Masasi Mkoani Mtwara kwa ajili ya maziko yanayofanyika kesho tarehe 29, kijijini kwao Lupaso.