Jumanne , 5th Mei , 2015

Mgomo ulioanza jana ambao umeendelea leo umeathiri shughuli za biashara na kiuchumi nchini Tanzania ambapo pia sekta ya ajira imeathirika kutoka na wafanyakazi kushindwa kufika maofisini kwa wakati.

Mabasi ya Abiria yakiwa yamepaki baada ya Mgomo wa Madereva.

Akizungumza na East Africa Radio Mwenyekiti wa Chama cha wamiliki wa Daladala DACOBOA, Sabri Mabruk amesema kutochukuliwa kwa hatua za haraka za kufanya mazungumzo na madereva kumepelekea kuleta usumbufu mkubwa kwa abiria huku wao wakikosa mapato kutokana na madereva kushinikiza mgomo kuwa wa lazima hata kwa ambao hawapo tayari kugoma.

Huko Jijini Arusha kamanda wa polisi Mkoani Arusha, Liberatus Sabasi alilazimika kukaa kwa masaa zaidi ya mawili, standi kubwa ya mabasi na kuwalazimisha wenye mabasi makubwa waliogoma, kuyaondoa magari hayo kwa haraka kabla ya kuyavuta kituo cha Polisi na jeki maalum ya kuvuta magari.

Wakati hayo yakiendelea katika mikoa Tofauti jijini Dar es Salaam Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda ameunda kamati maalumu ya kudumu ya kusimamia usafiri wa barabarani nchini ili kutatua changamoto zinazoikabali sekta ya Usafiri.

Akiongea kwa niaba ya waziri mkuu, waziri wa uchukuzi Samweli Sitta amesema kamati iliyoundwa inatakiwa kuanza kufanya vikao kuanza jana na kila mwezi watakutana kujadili na kutatua changamoto zote ikiwa ni pamoja na kasoro za kisheria ambazo zitapelekwa serikalini kwa mchakato zaidi wa kuzirekebisha.