Jumatano , 13th Jan , 2016

Baadhi ya viongozi wa siasa nchini wametaka wigo wa mazungumzo ya mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar upanuliwe kwa kushirikisha wadau wote badala ya kuviachia vyama vinavyovutana vya CCM na CUF peke yao.

James Mbatia ni mmoja wa Viongozi wa Umoja wa UKAWA, na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi ambaye jana ametoa maoni juu ya mgogoro wa Zanzibar

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi, Mhe. James Mbatia ametaka mgogoro huo kutatuliwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar pamoja na kuhusisha kituo cha demokrasia nchini ili kupata suluhusu ya suala hilo.

Mhe. Mbatia amesema kuwa mgogoro huo wa kikatiba usipotatuliwa na kufuata busara ya kuwahusisha wadau tofauti unaweza kusababisha machafuko visiwani humo na kuliharibia jina taifa pamoja na kugharimu maisha ya watanzania.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa chama cha Sauti ya Umma (SAU), Bw. Yusuph Manyanga amesema kuwa majadiliano ya vyama viwili kwa sasa hayalengi kutafuta suluhisho kutokana na kila chama kuvutia upande wake.