Jumatano , 17th Mei , 2023

Watu 65 wamethibitika kuuawa katika Mkoa wa Kagera katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Mei mwaka huu mwaka 2023 ikilinganishwa na watu 60 waliouawa katika kipindi kama hicho mwaka jana

Kamanda wa polisi mkoani Kagera ambaye sasa amehamishiwa Mkoa wa Kaskazini Pemba, William Mwampaghale amesema kuwa idadi hiyo haihusishi watu waliopoteza maisha kwa  kujinyonga, kuzama katika maji au kuchukuliwa na mamba

"Lakini kwa kipindi kama hiki mwaka jana, waliouawa walikuwa ni 60, hayapungui bali yanaongezeka, ndiyo maana nikaona kwa kuwa nilishapanga ratiba hii na bado sijakabidhi Mkoa kwa anayekuja, nipite kwa watendaji na wananchi tusemezane, nini kifanyike tuondokane na hili, maana kuongoza kwa mauaji sio jambo jema, linakwamisha hata maendeleo ya Mkoa" amesema Mwampaghale.

Nao baadhi ya Wananchi waliozungumza na EATV wamelishukuru jeshi la polisi kwa kuendelea kutoa elimu kwao juu ya namna ya kukabiliana na uhalifu, na kushauri waendelee kushirikiana nao.

"Lakini pia mambo ambayo ameelekeza yafanyiwe kazi, ikiwamo kuangalia namna ya kuwaondoa watoto wa mitaani kwa sababu pia ni sehemu ya ongezeko la uhalifu" amesema Pili Makunenge.