Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga.
Balozi Mahiga amesema kuwa kukosekana kwa utawala bora, changamoto za ugaidi, biashara za dawa za kulevya, biashara ya kusafirisha binadamu na uwepo wa rushwa na ufisadi ni baadhi ya mambo yaliyofanya dunia ibadilike.
Aidha Waziri huyo ameongeza kwa kusema kuwa masuala ya mazungumzo kuhusu rushwa zamani yalikuwa hayana mahali pa kuzungumzwa, kwa hiyo vikao kama hivyo vitasaidia kukabili tatizo hili.
Amesema kuwa mataifa mengi yangependa kuwemo katika harakati hizo lakini ni faraja kuona Tanzania ni miongoni mwa waanzilishi na hii ni kwa sababu ya uongozi na ujasiri wa Rais Dk. John Pombe Magufuli ambaye amebadili mwelekeo wa Taifa kwani ana utashi wa kisiasa na ana ujasiri wa kukemea maovu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Valentino Mlowola amesema vita ya rushwa nchini Tanzania ni endelevu na inafanyika kuitikia wito alioutoa Rais Magufuli wakati akizindua Bunge la Tanzania Novemba 20, 2015.
Mlowola amesema wanatumia mbinu mbalimbali kupambana na rushwa lakini kubwa wanayoenda nayo hivi sasa ni kutoa elimu kwa watoto na vijana ili kuwabadilisha tabia na utamaduni uliojikita kwenye jamii.