Alhamisi , 11th Dec , 2014

Wasafirishaji wa abiria mkoani Ruvuma wameaswa kutokuongeza nauli kiholela Katika kipindi hiki cha sikukuu ya krismas na mwaka mpya bila kufuata taratibu zilizowekwa na mamlaka ya udhibiti usafiri wa majini na nchi kavu SUMATRA.

Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Israel Sekirasa.

Akizungumzia matukio ya baadhi ya wasafirishaji wa abiria mkoani Ruvuma kuongeza nauli pasipo kufuata taratibu zinazowekwa na mamlaka husika katika kipindi cha sikukuu kwa visingizio mbali mbali huku lengo lao ikiwa ni kujipatia kipato zaidi na kuwanyonya abiria meneja wa mamlaka hiyo mkoani Ruvuma Sebastian Rohayi amesema mamlaka haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika watakaothibitika kufanya vitendo vya namna hiyo.

Amesema baadhi ya wasafirishaji wa abiria kwa kushirikiana na madereva na makondakta pamoja na wapiga debe wamekuwa na tabia ya kuongeza bei ya nauli kwa visingizio mbali mbali nyakati za sikukuu huku lengo lao kubwa ikiwa ni kujipatia maslahi zaidi na kuwanyonya wananchi kinyume na sheria na taratibu zilizowekwa na mamlaka.

Aidha Rohanyi amesema ili kuzuia vitendo hivyo vya kupandisha bei ya nauli wamiliki wanapaswa kukaa na kuzungumza madererva pamoja na makondakta ili kuwazuia kupandisha nauli na badala yake zitumike nauli zilizopangwa na mamlaka.

Amesema hatua zikazochukuliwa dhidi ya wahusika watakaothibitika kukiuka taratibu zilizopo ni kutozwa faini isiyopungua shili laki mbili na nusu au kusitishiwa leseni za usafirishaji kwa watakaothibitika katika utii wa sheria za usafirishaji wa abiria kwa sababu udhibiti huo unafanywa kwa ushirikiano na mamlaka nyingine za usafiri likiwemo jeshi la polisi kikosi cha usalama bara barani.