![](http://eatv.tv/sites/default/files/styles/detailpageimg/public/news/2025/02/15/TUNAENDA.jpg?itok=ap6JEhlP×tamp=1739631168)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Chama cha Mapinduzi kimeshamaliza mchakato wa kupata mgombea Urais wa Chama hicho katika uchaguzi Mkuu utakaofanya mwaka 2025.
Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi (Februari 15, 2025) wakati Mkutano Mkuu Maalum Chama cha Mapinduzi Jimbo la Itilima, uliofanyika katika uwanja wa Stand Mpya ya Itilima, mkoani Simiyu.
Waziri Majaliwa amesema kuwa kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi chama hicho kimewapa ridhaa ya kuendelea kuwatumikia Watanzania katika kipindi cha 2025-2030.
“Mama yupo na sisi, tunaye na tunaenda nae, Mwaka huu tumewaleta wagombea bora kabisa ambao wamethibitisha bila shaka kwamba utendaji wao umetukuka katika kipindi walichokuwa wanawatumikia watanzania”.
Amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia imeshuhudiwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imegusa moja kwa moja maisha ya Watanzania kwenye sekta za elimu, kilimo, afya, maji, miundombinu na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
“Chama cha Mapinduzi kina Sera imara zinazotekelezeka na watanzania wanakiamini Chama cha Mapinduzi, kinakubalika na ndicho kinachotumainiwa kutokana na uwezo wake wa hali ya juu wa kuwatumikia Watanzania, Mwaka huu tunalo jukumu la kuwaambia watanzania nini tumefanya na nini tutafanya katika kuwajibika na kusimamia maendeleo ya Watanzania”.