
Watu watano wakiwemo watatu wa familia moja, wakazi wa kata na kijiji cha Bulige halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, wamekufa baada ya kuzama kwenye dimbwi la maji, lililopo jirani na makazi yao.
Kwa mujibu wa mama aliyepoteza watoto wake wawili katika mkasa huo Prisca Luchagula, tukio hilo lilitokea siku ya jumammosi Februari 15, mwaka huu 2025, majira ya saa kumi jioni, wakati watoto wawili kati yao wakiwa wanatoka shambani na kuanza kuogelea katika dimbwi hilo.
Alisema wakati wakiendelea kuogelea maji yaliwazidi nguvu na kuwazamisha, hali iliyosababisha mama aliyekuwa jirani kutumbukia kwa lengo la kuwaokoa watoto hao ndipo nae akazama, huku watoto wake wawili waliokuwa pembeni nao wakaingia kutaka kumwokoa mama yao nao pia wakazama na kufariki.
Mwenyekiti wa kijiji cha Bulige Allen Mahanga, alisema dimbwi hilo ni miongoni mwa mashimo yaliyokuwa yakitumiwa na waanakijiji kuchimba madini ya ujenzi, kwa ajili ya ujenzi wa makazi yao.
Mkuu wa jeshi la zimamoto na uokoaji wilayani Kahama Stanley Luhwago, alithibitisha kupokea taarifa ya tukio hilo, na kuwataja waliokufa kuwa ni Zawadi Nkwambi(13), Khadija Nkwambi(11), Rahel Peter(11), Samike Peter(01) pamoja na mama mzazi wa Samike, Hoja Kubo(29) aliyefariki wakati akijaribu kuwaokoa wanae wawili.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kahama Mboni Mhita aliyefika katika kijiji hicho leo February 18, 2025, kwa lengo la kutoa pole kwa familia hizo, alitumia nafasi hiyo kutoa maelekezo kwa viongozi wa vijiji na vitongoji wilayani humo kuhakikisha wanayambua maeneo yote yenye madimbwi/mabwawa ya maji ili yalindwe kwa kuwekewa uzio, mlango wa kuingia na kutokea ili kuzuia maafa zaidi yasiendelee kutokea.
Sambamba na hilo, Mhita aliwataka Tarura na Tanroads, kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza miradi hususan ya barabara wilayani humo kuhakikisha wanatengeneza mazingira salama wanapomaliza shughuli zao ili kuzuia maafa yasitokee.