Jumatatu , 31st Oct , 2022

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt.Philip Mpango leo Oktoba 31 2022 amewasili Abidjan nchini Ivory Coast ambapo atamwakilisha Rais wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan katika jukwaa la uwekezaji barani Afrika litakalofanyika Novemba 02 hadi 04 mwaka huu.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akipokelewa Nchini Ivory Coast

Makamu wa Rais anatarajia kuongoza mazungumzo baina ya Tanzania na wawekezaji mbalimbali kuhusu uwekezaji katika miradi ya kimkakati nchini Tanzania katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji, usafirishaji na Uchukuzi.

Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika linaratibiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kushirikiana na waanzilishi wa jukwaa hilo na linalenga kuwakutanisha wawekezaji, sekta binafsi na sekta ya umma ili kuweka mikakati ya kufadhili miradi endelevu.

Jukwaa hilo linashirikisha wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, Wakuu wa taasisi na mashirika ya kimataifa pamoja na wafanyabiashara.