
Ajali hiyo imehusisha gari la abiria aina ya Hiace lenye namba za usajili T 294 DSS lililokuwa likitokea vijiji vya Sikaungu na Malonje kuelekea mjini Sumbawanga, ambapo katika mteremko mkali wa Kona ya Ulinji, gari hilo lilishindwa kudhibitiwa na kugonga bajaji yenye namba MC 416 BZQ iliyokuwa imeegeshwa kando ya barabara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, SACP Shadrack Masija, amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha ajali huenda ni kufeli kwa breki au dereva kutumia mwendo huru (neutral) katika eneo hilo hatarishi lenye mteremko mkali.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Sumbawanga, Dkt. Ismail Macha, amesema miili ya marehemu sita imepokelewa hospitalini, ambapo watatu kati yao ni watoto na watatu ni watu wazima. Aidha, kati ya majeruhi 21 waliopokelewa, wanawake ni 8 na wanaume 13, huku watatu wakiwa katika hali mahututi na kupelekwa chumba cha uangalizi maalum (ICU).