
Kwa mujibu wa shirika la utafiti la serikali ya Marekani Taasisi za Afya za Taifa (NIH), chanjo hiyo inayoitwa VIR-1388, imeundwa kusaidia seli za mwili T, hizi ni sehemu ya mfumo wa kinga na kufanya doria na kukagua seli zingine kwa matatizo.
Chanjo hiyo inalenga kuuelekeza mfumo wa kinga ya mwili kuzalisha seli za T "ambazo zinaweza kutambua VVU na kuashiria kinga ya mwili ili kuzuia virusi kuanzisha maambukizi sugu".
Majaribio ya chanjo hiyo yanafadhiliwa na NIH, mfuko wa Bill na Melinda Gates na kampuni ya Marekani ya Vir Bioteknolojia.
Utafiti huo utawaandikisha washiriki 95 wenye VVU katika maeneo manne nchini Afrika Kusini na maeneo sita nchini Marekani.
Matokeo ya awali ya majaribio ya chanjo yatatangazwa mwishoni mwa 2024, lakini baadhi ya washiriki wataendelea na majaribio kwa miaka mitatu.
Mwaka 2020, NIH ilisitisha majaribio ya chanjo nyingine ya VVU nchini Afrika Kusini baada ya uchunguzi kubaini kuwa chanjo hiyo haina ufanisi katika kuzuia maambukizi ya VVU.