RAIS, Dk .John Magufuli leo amewatunuku Kamisheni kwa Cheo cha Luteni Usu, Maafisa Wanafunzi Wapya 205 pamoja na kutoa Nishani kwa Maafisa watano waliofanya vizuri kwenye masomo yao.
Rais alitoa Kamisheni hiyo kwa Cheo cha Luteni Usu leo, katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA) ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu akiwa Rais.
Miongoni mwa Maafisa hao wapya watano waliotunukiwa nishani zao ni wanawake wawili ambao ni Efrasia Bundala kutoka Tanzania na Winnie Indumuli kutoka nchini (Kenya) huku wanaume wakiwa watatu ambao ni Phinias Kiganga aliyefanya vyema darasani.
Wengine ni Frank Kitalekwa aliyefanya vyema upande wa medani na Ahmed Mmang'anda aliyefanya vyema darasani.
Baada ya kuwavisha nishani askari hao watano ambao ni miongoni mwa maafisa wapya 205, Rais Magufuli aliwatunuku Kamisheni kwa cheo cha Luteni Usu maafisa hao wapya ambao miongoni mwao wanawake ni 16 na wanaume wakiwa 189.
Aidha miongoni mwa wahitimu hao wawili wanatoka nchini Burundi, 4 nchini Kenya na 4 wanatoka nchini Uganda ambao ni nchi marafiki.
Mara baada ya kutoa kamisheni kwa maafisa hao, Rais Magufuli alipata burudani kutoka kwa Kikundi cha Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) Oljoro ambao walipokuwa wakiimba walimpongeza Rais Magufuli kwa utendaji wake wa kazi na kumuomba kusafisha wabadhirifu wote wakwepa kodi pia asafishe taasisi mbalimbali ili Tanzania iwe safi.
Nayo bendi ya Jeshi la Watanzania(JWTZ) iitwayo Chacharika Bendi ilikonga nyoyo za wananchi waliofurika kushuhudia ndugu zao waliotunukiwa Kamisheni zao huku wakimpongeza kwa utoaji wa elimu bure.
Pia alipiga picha na maafisa hao wapya, viongozi mbalimbali.
Awali akiingia uwanjani kwa ajili ya ukaguzi wa gwaride Rais Magufuli alishangiliwa na wananchi mbalimbali waliohudhuria sherehe hiyo lakini pia viongozi wa serikali pamoja na wageni waalikwa waliohudhuria katika sherehe hiyo.