
Rais ametia saini nyaraka hizo Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma. Msamaha huo aliutoa jana Jumamosi Desemba 9,2017 katika maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara). Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kazi nzuri ya kurekebisha tabia za wafungwa.
Taarifa ya Ikulu imesema Rais Magufuli amesisitiza kuwa pamoja na kutolewa msamaha huo, vyombo vya dola viendelee kusimamia sheria.
“Nimeona nitumie kifungu hiki cha Katiba - Ibara ya 45 (1) ambacho nilipewa na Watanzania, ingawa kilikuwa hakijawahi kutumika, unajua mtu ambaye alihukumiwa kunyongwa halafu baadaye anaachiwa, ni kitu kinashangaza kwa sababu hakijawahi kutokea, lakini nimeona nifanye hivyo kwa ajili ya Watanzania,” amesema.
Ameongeza, “Muendelee kusimamia wajibu wenu na kusimamia sheria, mtu anayehukumiwa kufungwa afungwe kweli, na nilishatoa wito kwa magereza, pasiwepo wafungwa wa kukaa tu na kupumzika, wafanye kazi, kufungwa si kustarehe.”
Akizungumzia hilo, Kamishna Jenerali wa Magereza Dk Juma Malewa amemshukuru Rais kwa kutoa msamaha huo wa kihistoria.
Amesema wafungwa na maofisa Magereza wameipongeza hatua hiyo ambayo itasaidia kuwatia moyo wafungwa wanaorekebishwa tabia katika magereza nchini na kuongeza kwamba wafungwa waliopatiwa msamaha wa kuachiwa huru, waliruhusiwa kutoka magerezani tangu jana.