Alhamisi , 30th Aug , 2018

Rais John Magufuli amewataka viongozi kujenga mazingira ya kuwatumikia wananchi bila kujali wapo kwenye nafasi gani na kuwataka wafanyakazi wasitumike kwa maslahi ya watu fulani.

Rais Dkt. John Magufuli akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda.

Magufuli ameyasema hayo leo Agosti 30, akizungumza na madiwani, viongozi na watumishi wa Halamshauri ya Wilaya ya Chato, Geita ambapo ametolea mfano sakata la makontena ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda yanayotarajia kupigwa mnada baada ya kushindwa kulipiwa kodi bandarini.

Amesema sheria za nchi zinasema wazi kuwa ni mtu mmoja tu katika nchi mwenye dhamana ya kutolipa kodi kwa mujibu wa sheria ya fedha, sheria ya madeni, sheria ya dhamana na ya misaada.

Rais Magufuli amesema kuwa hakuna mtu mwingine zaidi ya aliyeruhusiwa kwa mamlaka aliyopewa, “Sasa ukichukua makontena kule, umezungumza na watu wengine labda na wafanyabiashara, unasema ni makontena yako, halafu ukasema tena labda ni ya walimu, wala hata shule hazitajwi, Maana yake nini?”

Ameongeza kuwa, “Maana yake si unataka utumie walimu, ulete haya makontena, utapeleka shule mbili au tatu, ndizo zitapewa mengine unakwenda kuyauza unapeleka kwenye shoping mall. Lakini walimu walikuambia wanahitaji makochi, sofa”.

Hayo yamejiri baada ya kuwepo kwa mvutano juu ya makontena hayo bandarini hali iliyopelekeaTRA kuchapisha tangazo kwenye gazeti la serikali la Daily News Mei 12, liliwataka wamiliki wa mali zilizokaa bandarini kwa zaidi ya siku 90 kujitokeza kuzilipia. Pia liliwataka wamiliki kuitoa mizigo hiyo ndani ya siku 30 kuanzia siku ilipotangazwa.

Tayari Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ameagiza makontena 20 ya samani yaliyoingizwa nchini na Makonda, yapigwe mnada ikiwa ni sehemu ya kusimamia sheria na kanuni za kodi zilizopo nchini.