Mzee Ibrahim Amani ambaye aliwahi kuwa Waziri na Mjumbe wa baraza la Mapinduzi Zanzibar, ni mmoja wa Watu 14 waliojitoa muhanga kupambana na kuuondoa utawala wa kisultani huko Tanzania Zanzibar, na kuondoka kwake kunafanya idadi ya wanapinduzi waliotangulia mbele za haki kufikia 13.
Katika Salamu zake, Rais Magufuli amesema kwa mara nyingine Taifa limepoteza mtu muhimu, Mzalendo wa kweli na ambaye daima alisimama kidete kutetea Taifa lake dhidi ya vitendo vyenye kuleta madhara.
"Nimeguswa sana na kifo cha Mzee Ibrahim Amani, maisha yake na nia yake ya kupigania uhuru na uzalendo kwa taifa lake ni mambo ambayo daima tutayaenzi" Amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli amemuomba Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein kumfikishia salamu za pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na kifo cha Mzee Ibrahim Amani.
"Tumwombe Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Ibrahim Amani mahali pema peponi, Amina." Amemalizia Rais Magufuli.