Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema
Lema ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na EATV kuhusu uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi wa jimbo lake ikiwa ni moja ya ahadi zake wakati wa kuomba kura ambapo kwa kuanzia kwa sasa ametoa gari la kubebea wagonjwa katika kituo cha afya Mwivaro.
''Nilipoanza kuwa Mbunge mwaka 2010 Halmashauri ilikuwa inakusanya shilingi milioni 200 kwa mwezi tukaendesha harakati za kumpata Meya wa upinzani ili kukusanya mapato zaidi na sasa hivi tunakusanya karibia shilingi bilioni 2 na lengo letu ni kufikia shilingi bilioni 2.5 kwa mwezi na tukifikia hapo tutakuwa na wigo mpana wa kuhudumia wananchi zaidi katika miradi ya maendeleo,'' alisema Lema.
Jiji la Arusha linaongozwa na Meya kutoka Chadema Bw. Kalisti Lazaro ambaye ni Meya wa kwanza kutoka upinzani kuongoza Halmashauri ya Jiji la Arusha kuanzia kuanza kwa uchaguzi wa vyama vingi mwaka 1995 ambapo anakabiliwa na mtihani wa kuonyesha utofauti kati ya uongozi uliopita na wa kwake hasa katika kuleta maendeleo katika Jiji la Arusha.



