Jumanne , 22nd Aug , 2023

Kamishna Mkuu wa Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Dr. Fredy Manongi amesisitiza kuwa nia ya serikali kuwatoa waliokuwa wanaishi katika hifadhi ya Ngorongoro ilikuwa ni sababu za kibinadamu na sio kuwajali wanyama zaidi ya watu kama inavyoelezwa

Katika mkutano wa mtandaoni uliowakutanisha wadau mbalimbali kuhusu awamu ya pili ya kuwahamisha wananchi wanaoishi hifadhini hapo kwenda Msomera mkoani Tanga Dr. Fredy amesema kuwa kumekuwepo na upotishaji juu ya zoezi hilo ila wanaendelea kutoa elimu

"Kweli maisha ndani ya hifadhi ni duni, nadhani mtu yoyote atakubaliana na mimi kwamba maisha ndani ya hifadhi ni magumu sana kwa wenyeji, na maendeleo na maendeleo ni magumu, kwa hiyo kwa nia njema serikali ikaona ihamishe hao watu"

"Kuwatoa watu ndani ya hifadhi sababu kubwa ilikuwa ni maisha ya watu na wala sio wanyama, watu wanasema tyunajali sana wanyama kuliko binadamu, lakini sababu kubwa ilikuwa ni maisha ya binadamu ili tuyaboreshe" 

"Muitikio wa watu kuhama Ngorongoro ni mkubwa, bado kuna wapotoshaji kama ilivyo kawaida, lakini tunajaribu kudhibiti hiyo hali ambayo sisi tunadhani hawatendi haki" amesema Dr. Fredy Manongi, Kamishna Mkuu wa Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) 

Kwa upande wake Prof. Hamis Masanja Malebo ambaye ni Katibu Mtendaji Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa changamoto katika maeneo ya hifadhi zimekuwa nyingi ikiwemo watoto kushindwa kwenda shule kwa sababu ya wanyama wakali hivyo uamuzi wa serikali ulikuwa sahihi

"Changamoto katika maeneo ya hifadhi ni kwamba kuna wanyama wanaokula nyama, kuna simba, chui, fisi, hawa watatu ni wanyama ambao hawana urafiki na binadamu, na wao wanawinda wanyama wote wanaopatikana katika eneo la hifadhi akiwemo binadamu" 

"Ugumu wa kuwapa huduma wananchi wa Ngorongoro unawafanya waendelee kuteseka na magonjwa ambayo yanadhibitika, ni kweli kabisa magonjwa yapo na sehemu nyingine lakini kiwango cha magonjwa kwa Ngorongoro ni kikubwa" 

Naye Elibariki Bajuta, Naibu Kamishna Uhifadhi na Utalii na Maendeleo ya jamii Ngorongoro amesema kuwa upotoshaji kuhusu zoezi hilo umekuwa ukiwakwamisha sana lakini elimu zaidi inaendelea kutolewa kwa wananchi 

"Kuna watu ambao wanaona zoezi hilo lina manufaa kwa jamii lakini kuna watu ambao wanaona zoezi hili sio nzuri, kuna baadhi ya watu wamekuwa wakipotosha, kwa kweli imesababisha sana kuweko kwa mkwamo kwa sababu mtu anataka kuhama anaposikia tena stori nyingine inamfanya asitake kuhama kwa kweli upotoshaji unakwamisha sana zoezi"