
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George Simbachawene amesema katika utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli ifikapo tarehe 30 mwezi Juni shule zote nchini ziwe na madawati ya kutosha ofisi yake imeanza kukusanya ripoti ya nchi nzima ambayo itaonyesha namna ya utekelezaji wa agizo hilo unavyofanyika.
Waziri Simbachawene ameyasema hayo leo katika mahojiano maalum na East Africa Radio na kusema katika kuhakikisha zoezi hilo linatekelezwa kwa wakati ofisi yake imeshaagiza watendaji wa ngazi zote kwa kila eneo kuhakikisha wanakusanya ripoti ambayo itawezesha serikali kuweka mipango ya kuongeza nguvu katika upatikanaji wa madawati kwa maeneo ambayo yamekosa huduma hiyo.
Amesema madawati yanayotengenezwa yawe na uwezo wa kuhimili mazingira ya wanafunzi ili yaweze kudumu kwa muda mrefu sambamba na hilo serikali imehimiza ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuhakikisha madawati hayo yanayotengenezwa yaweze kutunzwa kwenye mazingira salama na kukaa kwa muda mrefu.
Ametoa wito kwa watanzania wote bila ubaguzi wajitolee katika kuchangia elimu ya nchi yetu kwakuwa sekta ya elimu ni eneo ambalo linawekeza hazina kubwa ya nguvu kazi ya taifa kwa baadaye.
Ofisi ya Rais TAMISEMI inatarajia kutoa ripoti ya utekelezaji huo siku ya tarehe 1 Juni mwaka huu.