Jumamosi , 9th Apr , 2016

Vijana waliohitimu elimu ya juu hapa nchini wameshauriwa kutumia elimu yao katika kujiajiri hasa kwenye sekta ya kilimo biashara ambayo imekuwa ikikua siku hadi siku na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira.

Balozi wa Denmark nchini Tanzania Bw. Eina Jensen ametoa ushauri huo leo jijini Dar es salaam wakati alipokuwa akizindua kampuni mbili za masuala ya kilimo zilizotokana na vijana wahitimu wa ushirika wa wajasiriamali wa chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine ambao wameweza kubuni bidhaa kwa kutumia mazao ya ndani.

Naye Bwana Revocatus Kimario wa shirika la ujasiriamali la wahitimu wa chuo cha Sokoine SUGECO amesema vijana wajitengenezee ajira na kuwaajiri wengine kwa kutumia matatizo yaliyopo kwenye soko la kilimo ambalo kwa muda mrefu hayajapatiwa ufumbuzi.

Kimario amesema Kilimo kinawategemea, wasomi wa fani ya biashara, uhandisi na teknologia ili kufanya mageuzi ndani ya sekta ya kilimo jambo ambalo litaongeza upatikanaji wa ajira za uhakika na kuinua uchumi.