Ijumaa , 27th Feb , 2015

UKATILI wa Kijinsia unaongoza Mkoa wa Kilimanjaro ni wa utelekezaji familia, ambapo akina baba huwafukuza wake zao na watoto bila kujali watalala na kula wapi, jambo linalochangia ongezeko la watoto wa mtaani.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama.

Akizungumza jana Mjini Moshi na waandishi wa habari waliokuwa katika mafunzo ya siku tatu yalioandaliwa na Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kuhusu uandikaji wa matukio ya ukatili wa kijinsia, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia Mkoa huo, Priscal Maganga, amesema wanaume mkoani humo wanaongoza kutelekeza familia zao.

Amesema katika kipindi cha miezi miwili ya Januari hadi Februari mwaka huu, wamepokea kesi 20 za utelekezaji familia.

Priscal amesema wanawake hao na watoto wanapofukuzwa wanakimbilia katika dawati hilo wakiamini watapata fedha na msaada mwingine, ila nao polisi hawana fungu la kusaidia, wanachofanya ni kuchangishana ili umsaidia muhusika.

Amesema kuwa hata hivyo kwa sasa kesi hizo zimepungua kwani miaka ya nyuma walikuwa wakipokea kesi 50 kwa mwezi, jambo lililowalazimu kutoa elimu kwenye mikusanyiko ya watu ili kuelimisha jamii na kueleza madhara ya kutelekeza familia mabaya.

Aidha amesema kuwa upande wa ukatili wa kubaka, wamepokea kesi tano katika kipindi cha miezi hiyo, huku kesi za kulawiti ziko tatu na ukatili dhidi ya mtoto, ambaye alipigwa na wazazi wake kupita kiasi ipo moja.