Jumamosi , 2nd Mei , 2015

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWENYE KILELE CHA SIKUKUU YA WAFANYAKAZI DUNIANI, MEI MOSI, 2015 MWANZA

Nakushukuru sana Rais wa TUCTA Ndugu Gratian Mukoba na viongozi wenzako wa vyama vya wafanyakazi kwa kunialika kuja kushiriki nanyi katika sherehe za mwaka 2015 za Mei Mosi hapa Mwanza. Aidha, natoa pongezi nyingi kwa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi na Ujenzi Tanzania (TAMICO) ambao ndio wenyeji wetu mwaka huu kwa maandalizi mazuri ya Sherehe hizi. Hakika yamefana sana.

Sote ni mashahidi wa jinsi maandamano na maonesho ya kazi za wafanyakazi wa Tanzania yalivyopendeza. Nimesoma mengi ya mabango ya waandamanaji, napenda kuwahakikishia kuwa ujumbe umefika.

Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza ndugu zetu wa Mkoa wa Mwanza wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Ndugu Magesa Mulongo kwa kukubali kuwa wenyeji wa maadhimisho ya sherehe hizi. Mmetupokea vizuri na kutukirimu kwa heshima kubwa. Tunajisikia tuko nyumbani.

Ndugu Rais wa TUCTA;
Kwa mara nyingine tena nakupongeza kwa kuchaguliwa kwako kuwa Rais wa TUCTA. Sisi katika Serikali tumeupokea kwa furaha uchaguzi wako. Narudia kukuhakikishia ushirikiano wangu na wa wenzangu wote katika Serikali ninayoiongoza, katika utekelezaji wa majukumu yako. Ni matumaini yetu kuwa tutashirikiana kwa ukamilifu katika kuendeleza maslahi na ustawi wa wafanyakazi wa Tanzania na nchi yetu.

Ndugu wafanyakazi;
Napenda kuchukua nafasi hii kuwapa pole kwa msiba mkubwa mlioupata wa kuondokewa na Bwana Erasto John Kihwele aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU). Hakika mmepoteza kiongozi mahiri katika kujenga hoja na kupigania haki za wafanyakazi wa reli. Namkumbuka sana kwa jinsi alivyosimama kidete kutetea wafanyakazi wa TAZARA katika kikao chetu cha pamoja mwaka jana. Utetezi wake ulizaa matunda kwa kuanzishwa kwa Baraza la Wafanyakazi TAZARA. Kwa kweli sote tumepata pigo. Nawaomba muendeleze yale mazuri aliyoyasimamia. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi”. Ameen.

Pongezi kwa Wafanyakazi Bora
Ndugu Wafanyakazi;
Kama ilivyo ada leo tena tunawapongeza wafanyakazi wenzetu waliotekeleza vizuri majukumu yao katika maeneo yao ya kazi. Tunawapongeza kwa kazi yao njema iliyowawezesha kuibuka washindi kati ya wafanyakazi wengi walio bora. Nawapongeza na kuwasihi waendelee na ari na moyo huo wa kuchapa kazi kwa bidii, nidhamu na maarifa. Ni matumaini yangu kuwa mafanikio yao yatakuwa kichocheo kwa wengine kuongeza bidii zaidi ili waweze kufikia na hata kuzidi viwango vyao vya ubora mwakani.
Risala ya Wafanyakazi

Ndugu Rais wa TUCTA na Wafanyakazi Wenzangu;
Nimeisikiliza na kuifuatilia kwa makini sana risala ya wafanyakazi iliyowasilishwa kwa ufasaha na Katibu Mkuu wenu mahiri, Ndugu Nicholas Mgaya. Nawapongeza kwa risala nzuri iliyobeba maneno ya shukrani, changamoto, faraja na karaha za wafanyakazi. Risala yenu pia imekuwa na maoni yakinifu kuhusu namna ya kuyapatia ufumbuzi baadhi ya matatizo yaliyotajwa.

Nataka kuwahakikishieni kuwa nimeisikiliza neno kwa neno na kituo kwa kituo. Nimeyasikia yale mliyosema kwa uwazi na hata yale mliyoyasema kwa mabano. Nimeyapokea, tumeyapokea na kama ilivyo kawaida yetu tutayashughulikia kwa uzito unaostahili. Baadhi yake nitayazungumzia katika hotuba yangu hii.

Kauli Mbiu
Ndugu Rais wa TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi;
Nimefurahishwa na kauli mbiu ya Sherehe za mwaka huu isemayo “Jiandikishe, kura yako ni muhimu kwa maendeleo”. Kauli mbiu hii ni muafaka kabisa na wakati tulionao sasa. Ni kauli mbiu inayokumbusha wajibu muhimu wa kila mfanyakazi na kila Mtanzania.

Kupiga kura kuchangua viongozi na, kwa ajili ya kuamua mambo muhimu kitaifa, yanayotakiwa kuamuliwa kwa Kura ya Maoni kama ilivyo Katiba Inayopendekezwa, ni haki na wajibu wa msingi wa raia. Lakini, ili mtu aweze kuitumia haki yake hiyo na kutimiza wajibu wake huo lazima awe na kitambulisho cha mpiga kura. Kitambulisho hicho hupatikana kwa kujiandikisha katika Daftari la Mpiga Kura.

Naungana nanyi kuwahimiza wafanyakazi mjitokeze kujiandikisha pale mtakapotangaziwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya hivyo. Ni muhimu sana kuitumia fursa hiyo vizuri kwani haitarudi itakapopita. Narudia kukumbusha kuwa watakaopiga kura mwaka huu ni wale tu wenye vitambulisho vipya vya mpiga kura. Vya zamani havitambuliki.

Ndugu wafanyakazi;
Ni ukweli usiopingika kuwa maendeleo yanategemea kuwa na Katiba nzuri na viongozi wazuri. Hivyo basi, usiipoteze fursa hii adhimu kwa ajili ya kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa na kuchagua Rais, Mbunge, Mwakilishi na Diwani unayemuona anafaa. Hali kadhalika, ninyi mna ndugu, marafiki na kama viongozi wa kaya mnao wategemezi majumbani mwenu ambao wengine wanazo sifa za kuwa wapiga kura. Nawaomba muwakumbushe na kuwahimiza wajitokeze kujiandikisha na siku ikifika waende kupiga kura.

Ndugu Rais wa TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi;
Hii ndiyo sherehe ya Siku ya Wafanyakazi ya mwisho kwangu kuhudhuria nikiwa Rais wa nchi yetu. Nimekuwa nanyi kwenye maadhimisho haya kila mliponialika. Katika miaka 10 ya uongozi wangu tumefanya jitihada kubwa kukuza ajira na kuinua hali za wafanyakazi nchini. Nafarijika sana kuona kuwa naondoka wakati ambapo tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuyatekeleza yale tuliyopanga kufanya.

Ndugu Rais wa TUCTA;
Leo hii tukitazama tulikotoka na tulipo sasa tunaiona tofauti kubwa. Ninaposema hayo sina maana kuwa matatizo na changamoto zote za wafanyakazi zimekwisha. La hasha! Natambua pia kuwa isingelikuwa rahisi kumaliza mambo yote yanayowasibu wafanyakazi katika kipindi hiki. Tunachojivunia, ni kule kuweza kuzishughulikia kwa ufanisi changamoto za msingi za wafanyakazi. Hata hivyo ni muhimu kutambua kuwa bado tunayo kazi kubwa ya kufanya mbele yetu. Katu tusibweteke na kulevywa na mafanikio haya. Hatujafika katika safari yetu. Madamu tuko katika mwendo, tutafika.

Kuboresha Mazingira ya Kazi
Ndugu Wafanyakazi;
Kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali yetu tumefanikiwa kujenga taasisi, mifumo na sheria zinazoweka misingi imara ya utatuzi wa changamoto za wafanyakazi. Tumetunga Sheria na Kanuni mbalimbali kwa lengo la kulinda haki za msingi za wafanyakazi pamoja na kuweka mazingira bora ya kazi ikiwemo uhusiano kati ya waajiri na waajiriwa. Sheria na Kanuni hizi ni zile zinazohusu viwango vya kazi, hifadhi ya jamii, na ajira. Kanuni za kutekeleza Sheria ya Ajira na Mahusiano Na.6 ya 2004 zilitengenezwa na kuanza kutumika mwaka 2007.

Kuanza kutekelezwa kwa Sheria hii kumewezesha kuanzishwa na kuimarishwa kwa Taasisi mbalimbali za kazi, zikiwemo Idara ya Usimamizi Kazi na Huduma za Ukaguzi (Idara ya Kazi), Usajili wa Vyama vya Waajiri na Wafanyakazi, Mahakama ya Kazi, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wa Migogoro ya Kikazi (CMA), Bodi za Mshahara za Kisekta, Kamati ya Huduma Muhimu (Essential Services Committee) ya CMA na Baraza la Ushauri la Kazi, Uchumi na Jamii (LESCO). Kuwepo kwa vyombo hivi kumesaidia sana kuweka uwanja wa majadiliano kuwa sawa kati ya waajiri na waajiriwa.

Ushirikishwaji wa Wafanyakazi
Ndugu wafanyakazi;
Tangu tulipoingia madarakani katika awamu hii, tumetoa kipaumbele cha juu katika kuhakikisha kwamba ushirikishwaji wa Wafanyakazi unakuwa sehemu ya utamaduni katika sehemu za kazi. Kwa maneno mengine ni kwamba tumesisitiza utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6 ya 2004.

Juhudi zetu hizo zimezaa matunda. Tumeshuhudia Vyama vya Wafanyakazi vikiongezeka kutoka vyama vya Wafanyakazi 18 hadi 30 ambavyo vimesajiliwa ili kutetea maslahi ya Wafanyakazi. Aidha, Mashirikisho mawili (2) na Chama cha Waajiri kimoja (1) vimesajiliwa. Kwa lugha nyepesi tumewapa wafanyakazi sauti juu ya maslahi, hatima na mustakabali wao. Hata kwenye Bunge la Katiba wafanyakazi walishirikishwa kwa ukamilifu.

Mabaraza ya Wafanyakazi
Ndugu wafanyakazi;
Kwa upande wa utumishi wa umma, takwimu zinaonyesha kwamba Mabaraza ya Wafanyakazi yameundwa katika Wizara zote 26; Idara za Serikali 19; Wakala za Serikali 25 na Mamlaka za mikoa 21 na Halmashauri za Wilaya na Miji 168. Mengi ya Mabaraza hayo yamekuwa yanakutana kwa mujibu wa taratibu zilizopo. Hata hivyo zipo Idara za Serikali 4; Wakala za Serikali 7; Mikoa 5; na Mamlaka za Serikali za Mitaa 34 bado hazijaunda Mabaraza hayo kwa sababu mbalimbali.

Nimemuelekeza Waziri wa Kazi na Ajira na Katibu Mkuu Kiongozi wawabane wale wote ambao bado hawajaunda Mabaraza ya Wafanyakazi ili wafanye hivyo bila kuchelewa zaidi. Pia, kwa wote, waliounda Mabaraza na wale wote watakaounda ihakikishwe kuwa mabaraza hayo yanakutana mara mbili kwa mwaka kama Sheria inavyotaka. Kisingizio cha uhaba wa fedha hakiniingii akilini hata kidogo. Mbona sijawahi kusikia viongozi wamekosa posho za safari na vikao vyao! Hayo ni matakwa ya kisheria, na ni agizo la Rais hivyo lazima kupewa kipaumbele katika utekelezaji.
Ndugu wafanyakazi;

Jambo jingine zuri ambalo tumelifanya kwa ufanisi katika kipindi hiki ni kuwa na utaratibu wa Rais kukutana na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi. Tulianza kwa kukutana mara moja baadae tukaongeza na kuwa mara mbili kwa mwaka. Japo wakati mwingine imekuwa sio rahisi sana kukutana mara mbili kwa sababu ya ratiba za Rais, lakini hatukukosa kukutana angalau mara moja.

Mimi na viongozi wa vyama vya wafanyakazi ni shahidi kwamba vikao hivi vimesaidia sana kuleta maelewano baina ya Serikali na Vyama vya Wafanyakazi na hivyo baina ya Serikali na wafanyakazi. Vikao hivi vimekuwa fursa maalum ya kuzungumzia masuala mbalimbali yanayowahusu wafanyakazi na kuyatafutia ufumbuzi. Ukweli ni kwamba matatizo mengi tumeweza kuyatatua hata yale ambayo wakati mwingine yalionekana kuwa magumu sana.

Mwaka huu tumeshakutana mara moja. Ni matumaini yangu kuwa tutapata fursa ya kukutana tena, kabla sijang’atuka. Utakuwa mkutano wa kuagana. Nitamnong’oneza Rais ajaye kuhusu manufaa ya utaratibu huu, ili ikimpendeza auendeleze.

Huu ni utaratibu wa kisheria, umekuwa na manufaa makubwa sana. Kama mlivyosema, umesaidia kujenga maelewano mazuri na ushirikiano baina ya Serikali na wafanyakazi, jambo ambalo ni muhimu sana katika kuleta mustakabali mwema nchini. Naikumbuka pia ahadi yangu ya kukutana na viongozi wa Chama cha Waajiri. Nitatafuta wasaa hivi karibuni tukutane.

Usuluhishi wa Migogoro ya kikazi
Ndugu Wafanyakazi;
Katika awamu hii tumejitahidi sana kushughulikia migogoro ya kikazi kwa kupunguza muda wa mashauri kusikilizwa na hivyo kuwezesha wafanyakazi kupata haki zao kwa wakati. Kama nilivyosema awali, mwaka 2008 tulianzisha Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ambayo jukumu lake ni kushughulikia migogoro ya kikazi. Tangu kuanzishwa kwake Taasisi hii imefanikiwa kushughulikia migogoro ya kikazi 10,281 ambapo migogoro 6,057 imeshatolewa uamuzi. Tume imeweza kupunguza muda wa kusuluhisha na kusikiliza mashauri ya migogoro ya kazi kutoka wastani wa siku 30 hadi 12 na muda wa kuamua umepungua kutoka wastani wa siku 90 hadi 85.

Kupungua kwa muda wa mashauri kusikilizwa na kuamuliwa maana yake ni kupunguza usumbufu na madhila kwa mfanyakazi ambaye hapo awali alichelewa sana kupata haki yake. Wakati mwingine kuchelewa kupata haki kwa wakati kulitafsiriwa kama haki iliyodhulumiwa. Utaratibu huu umepunguza pia mlundikano wa kesi za masuala ya kazi mahakamani. Kasoro mlizozitaja katika risala yenu kuhusu utendaji wa CMA tutazifanyia kazi.

Usimamizi wa Ajira
Ndugu Wafanyakazi;
Kumekuwepo na malalamiko ya wafanyakazi juu ya kukithiri kwa idadi ya wageni wasio na sifa za kufanya kazi nchini ambao wanaajiriwa. Niliahidi katika hotuba yangu ya Mei Mosi mwaka jana kwamba tutatunga Sheria maalum na kuweka utaratibu wa kisheria wa kusimamia ajira za wageni nchini. Aidha, nilimwelekeza Waziri wa Kazi na Ajira akamilishe kanuni za kusimamia mawakala binafsi wa huduma za ajira.

Nafurahi kuwa ahadi yangu ile imetimia kwa kutungwa kwa Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni katika Bunge la Machi, 2015. Kilichobakia sasa ni Waziri wa Kazi na Ajira kutengeneza Kanuni za utekelezaji wa Sheria hiyo. Ningependa kazi hiyo ikamilike mapema ili Sheria ianze kutumika mapema iwezekanavyo.
Ndugu Wafanyakazi;

Kuhusu makampuni ya mawakala wa ajira, Serikali imekwishaweka utaratibu mzuri wa kuyatambua, kuyasajili upya na kuyatengenezea kanuni za kuongoza utendaji wao. Kwa ajili hiyo, hivi sasa Wizara inaweza kuyakagua na kujiridhisha iwapo yanafuata sheria za kazi. Tayari makampuni 96 yameshasajiliwa. Hata hivyo, ili shughuli hii iweze kufanikiwa ushirikiano wa wafanyakazi ni muhimu. Inasikitisha kusikia kuwa, wapo wafanyakazi wanaokataa kutoa taarifa za ukiukwaji wa Sheria unaofanywa na makampuni haya kwa kuogopa kupoteza ajira zao.

Napenda kuwahakikishia kuwa, Serikali itasimamia kwa nguvu zote utekelezaji wa jambo hili. Haitasita kuchukua hatua stahiki dhidi ya Mawakala watakaokiuka sheria za ajira nchini, watakapobainika kufanya hivyo. Tafadhalini timizeni wajibu wenu wa kutoa taarifa kuhusu wale wanaovunja Sheria na taratibu.

Hifadhi ya Jamii
Ndugu Wafanyakazi;
Katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne tumeboresha sana huduma ya hifadhi ya jamii ambayo ni moja ya haki za msingi kwa wafanyakazi. Hivi sasa tunaangalia uwezekano wa kujumuisha makundi mengine wakiwemo wakulima na wazee.

Mabadiliko ya kisheria na kisera tuliyochukua yameongeza wigo wa mafao, aina ya mafao na ongezeko la mafao kwa wafanyakazi. Takwimu zinaonyesha kwamba idadi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imeongezeka toka Mifuko 5 mwaka 2005 hadi mifuko 7 hivi sasa. Hali kadhalika, kumekuwepo na ongezeko kubwa la wanachama na wale wanaofaidika na huduma za hifadhi ya jamii hususan wafanyakazi na wategemezi wao. Idadi imeongezeka kutoka 690,000 mwaka 2005 hadi 6,400,000 mwaka 2014. Haya ni mafanikio makubwa sana.

Ndugu Rais wa TUCTA na wafanyakazi;
Habari nyingine njema ni kuwa hatimaye kile kilio chenu cha kutaka kuoanisha mafao ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuwa na kokotoo la aina moja kimepata ufumbuzi. Matokeo yake ni kwanza, kwamba mafao ya malipo ya pensheni ya mwezi sasa yameongezeka kwa asilimia 5 kutoka asilimia 67 hadi asilimia 72.5. Pili, ni kuwekwa kwa kiwango cha chini cha asilimia 40 ya mshahara hata kwa mwanachama ambaye pensheni yake ingekuwa chini ya asilimia 40 ya mshahara. Hii ina maana kuwa hakuna mwanachama wa mfuko wowote atakayepata pensheni ya chini ya asilimia 40 ya mshahara hata kama kwa masharti ya mfuko wake kabla ya uamuzi huu angestahili kupata chini ya hapo. Uamuzi huu unajenga usawa wa mafao kwa wanachama wote wa mifuko yote.

Ndugu Wafanyakazi;
Napenda kusisitiza kuwa mabadiliko haya hayataathiri wanachama wa mifuko ya PSPF na LAPF ambao waliajiriwa kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa ukokotoaji tulioanza tarehe 1 Julai, 2014. Najua ipo hofu fulani ambayo na hata katika mkutano wangu na viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi ilijitokeza (na leo pia imeelezwa kwenye risala yenu). Tulikubaliana mazungumzo zaidi yafanyike kati ya TUCTA na SSRA kuhusu jambo hili. Hivyo nawaomba muwe na subira. Heri itapatikana kama walivyosema Wahenga.

Nafurahi kutoa taarifa kuwa ufumbuzi umepatikana kuhusu suala la mafao kwa wale wafanyakazi ambao wakati wa utumishi wao, kabla ya kustaafu walichangia mifuko tofauti. Hawa ni wale ambao walihama au kuhamishwa kutoka Halmashauri za Wilaya na Miji na kwenda Serikali Kuu au kinyume chake. Kwa sababu hiyo wamechangia katika mifuko tofauti. Wanapostaafu wamekuwa wanapata ugumu katika malipo na kujikuta wanapoteza haki na stahili za utumishi wao wa muda mrefu. Mwongozo wa kuunganisha michango ya wanachama waliochangia katika mfuko zaidi ya mmoja umeshatolewa na umeanza kutumika tangu tarehe 25 Aprili, 2014. Tatizo limemalizika na tayari SSRA imeshatatua malalamiko ya wanachama wapatao 11,070 waliokuwa wamekabiliwa na matatizo ya namna hii.

Mfuko wa Fidia
Ndugu Wafanyakazi;
Kile kilio cha siku nyingi cha fidia ya wafanyakazi wanaoumia kazini nacho kimefutwa machozi. Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi (Workers Compensation Fund) umeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Fidia ya Wafanyakazi Na.20 ya mwaka 2008. Nimeshafanya uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko Ndugu Masha Mshomba na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Ndugu Emmanuel Humba. Waziri wa Kazi na Ajira ameshateua Wajumbe wa Bodi hivyo kazi imeanza. Kazi inayoendelea sasa ni kuandaa kanuni za uendeshaji wa Mfuko huo zinazotarajiwa kukamilika Juni, 2015.

Kama nilivyosema mwaka jana, Mfuko huu utachangiwa na waajiri wote yaani Serikali na wa sekta binafsi. Mfuko utaondoa ule mwanya wa baadhi ya waajiri kukwepa wajibu wa kulipa fidia pale yanapotokea madhara kwa wafanyakazi wao. Kwa hatua hii wafanyakazi sasa wana hakika ya kulipwa fidia stahiki.

Maslahi ya Wafanyakazi
Ndugu Rais wa TUCTA;
Wafanyakazi Wenzangu;
Jambo lingine ambalo tumejitahidi kufanya bila ajizi ni kuboresha maslahi ya wafanyakazi. Pamoja na changamoto tulizonazo kwa upande wa mapato na ukubwa wa majukumu ya serikali tumechukua hatua za makusudi kuongeza kima cha chini cha mishahara katika utumishi wa umma kila mwaka tangu tuingie madarakani. Kwa ajili hiyo, katika utumishi wa umma, kwa mfano, kima cha chini cha mshahara mwaka 2005 kilikuwa shilingi 65,000, mwaka 2014 kima cha chini kimeongezeka na kufikia shilingi 265,000. Ni nyongeza ya zaidi ya mara nne. Najua kwa hali ilivyo sasa ongezeko hili bado ni ndogo lakini si haba. Naahidi kuwa na mwaka huu pia tutaongeza.

Punguzo la Kodi kwa Wafanyakazi (PAYE)
Ndugu wafanyakazi;
Tumeendelea kupunguza kiwango cha kodi ya mapato kwa wafanyakazi (PAYE) mwaka hadi mwaka tangu 2005 hadi sasa. Kwa ajili hiyo, kodi hiyo iliyokuwa asilimia 18 sasa ni asilimia 12. Na mwaka huu pia tutaendelea kupunguza kodi ya mapato kwa wafanyakazi. Natambua kuwa maombi yenu ni kutaka iwe chini ya asilimia 10. Hatukuweza kufikia hapo mwaka huu lakini safari tuliyoianza na hapo tutakapofikia itabakisha padogo sana kufikia tunapopataka sote.
Ndugu Wafanyakazi;

Kama nilivyosema mwaka jana, kwa upande wa wafanyakazi katika sekta binafsi kima cha chini kinapangwa na Bodi za Mishahara za kisekta zinazoundwa na Waziri wa Kazi. Hadi kufikia mwaka 2011 tulikuwa nazo Bodi 12 ambazo zimewezesha majadiliano na waajiri wa sekta binafsi kufanyika. Matokeo yake ni kima cha chini cha mshahara kupanda kutoka shilingi 48,000 kwa mwezi hadi kati ya shilingi 100,000 na 400,000 kutegemeana na sekta. Kwa kuwa bodi hizo zinakutana kila baada ya miaka mitatu, na mara ya mwisho mishahara iliongezwa mwaka 2013 hivyo basi viwango vipya vinatarajiwa kutangazwa mwaka 2016.

Naambiwa kuwa bado wapo waajiri wasiolipa viwango hivi ambavyo vimekubaliwa kwa pamoja baina yao na wafanyakazi. Hili si jambo la kiungwana na linalonihuzunisha sana. Ndugu Almasi tusaidie tabia hii iachwe. Nazitaka mamlaka husika kutimiza ipasavyo wajibu wao wa kuhakikisha maamuzi ya Bodi yanatekelezwa. Tusikubali watu hao wakaendelea kudhulumu haki za wafanyakazi. Pendekezo la kutaka kuwepo na Bodi moja badala ya kila sekta kuwa na Bodi yake limepokelewa na litafanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA)
Ndugu Wafanyakazi;
Serikali yetu imetoa umuhimu mkubwa kwa uimarishaji wa afya ya wafanyakazi na usalama mahala pa kazi. Mafanikio makubwa yamepatikana. Kati ya mwaka 2010 na 2015 Wakala wa Afya na Usalama Mahala pa Kazi (OSHA) umefanya kaguzi za kawaida 26,000 na kaguzi maalumu 53,000. Hali kadhalika, wafanyakazi wapatao 435,063 wamepimwa afya zao kwa lengo la kubaini matatizo na athari wazipatazo wakati wakiwa kazini na hata baada ya kuacha kazi. Mwaka 2014, OSHA imefanya ukaguzi kwenye migodi yote nchini na kutoa maelekezo juu ya namna ya kuboresha hali katika migodi hiyo. Tutaendelea kuiimarisha OSHA ili iweze kufanya kaguzi nyingi zaidi na kwa wakati muafaka.

Marekebisho ya Miundo na Madai ya Wafanyakazi
Ndugu Wafanyakazi Wenzangu;
Katika kipindi cha miaka 10 hii, tumefanya marekebisho ya miundo ya utumishi ya kada mbalimbali za utumishi wa umma. Miundo miwili ninayopenda kuzungumzia leo ni ile ya walimu na wauguzi. Kwa upande wa walimu, muundo wa walimu umeidhinishwa na utekeleaji wake umeanza tangu Julai, 2014. Nimeambiwa kuwa utekelezaji haujaanza kote kwa wakati mmoja, lakini nimehakikishiwa kuwa wote watahamia kwenye muundo mpya katika mwaka ujao wa fedha.

Sambamba na hili la muundo, malimbikizo ya stahili za walimu yameendelea kulipwa. Mwaka huu madai ya deni la walimu yalikuwa shilingi bilioni 53,185,440,406 yanayowahusu na walimu 70,668 yalipokelewa. Uhakiki umefanyika na tayari, walimu 29,243 wamekwishalipwa jumla ya shilingi bilioni 23,233,654,025. Madai mengine ya walimu 7,169 ya jumla ya shilingi 9,285,283,600 yataanza kulipwa mwezi Agosti, 2015. Katika uhakiki uliofanywa, madai ya walimu 30,807 yenye thamani ya shilingi bilioni 17,346,593,468 yamekutwa na dosari na hivyo kurejeshwa kwenye Halmashauri na kwa wahusika kufanyiwa masahihisho. Napenda kuwahakikishia kuwa hizo zikirekebishwa malipo yatafanyika. Fanyeni hima jambo hili tulimalize.
Ndugu Rais wa TUCTA;

Tumekwishapeleka Bungeni Muswada wa Sheria ya kuanzisha Tume ya Utumishi wa Walimu (Teachers Service Commission) ambao tayari umesomwa kwa mara ya kwanza. Aidha, tunakamilisha maandalizi ya kuwasilisha Bungeni Muswada wa kuanzisha Bodi ya Taifa ya Taaluma za Walimu (National Teachers Professional Board). Yote haya yanathibitisha dhamira na utashi wetu kushughulikia masuala ya walimu na wafanyakazi kwa jumla. Shemeji zangu walimu baada ya kufanya hayo nina hakika nawaacha pazuri.
Nimefurahishwa na uamuzi wenu walimu wa kufungua Benki ya Walimu. Nawapongeza sana kwa hatua hii kubwa na ya maendeleo. Sisi katika Serikali tunaunga mkono juhudi za walimu na tunaahidi kutoa ushirikiano wa kuwezesha lengo lenu hili jema kutimia.

Ndugu Wafanyakazi;
Kwa upande wa kada ya wauguzi, mtakumbuka kuwa tulirekebisha muundo ambao umeanza kutumika tarehe 1 Julai, 2010. Tumepokea malalamiko kuwa mabadiliko hayo yameathiri baadhi ya wauguzi kwa viwango vyao vya mshahara kushuka baada ya kuanza kutumika kwa muundo mpya. Hili ni kosa ambalo halikustahili kutokea. Nimeelekeza lirekebishwe, mara moja. Nimeagiza wale ambao mishahara yao imeshushwa, warejeshewe mishahara yao ya awali na malimbikizo yao walipwe. Hali kadhalika, nafurahi kuwa yale maombi ya kutaka ianzishwe Kurugenzi ya kada ya wauguzi na wafamasiya nayo yamefanyiwa kazi. Kibali kimetolewa na Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa Kurugenzi hizo kuanzishwa. Kwa sasa ni kitengo.
Ndugu Wafanyakazi;

Katika kipindi hiki, tumeendelea kushughulikia na kufanikiwa kutatua kero nyingine nyingi za wafanyakazi. Kati ya mwaka 2005 na 2010, jumla ya watumishi 476,430 wamepandishwa vyeo. Aidha, kati ya mwaka 2012 na 2015, kwa mfano,jumla ya watumishi 125,372 wamelipwa malimbikizo ya jumla ya shilingi bilioni 123,141,755,959.68. Nimewaagiza ndugu zetu wa Hazina waanze kulipa madeni ya wafanyakazi wa Serikali za Mitaa yanayofikia shilingi bilioni 18,029,441,595.

Kwa kweli, mtakubaliana nami kuwa tumejishughulisha kwa kadri ya uwezo wetu kutafuta majawabu kwa kero na matatizo yanayowakabili wafanyakazi nchini. Hapajakuwako na upungufu wa dhamira upande wetu. Kwa yale ambayo hatukuweza kuyafanya ni kwa sababu ya ugumu wa tatizo lenyewe kulipatia ufumbuzi au kwa sababu ya uhaba wa pesa. Hakuna jambo ambalo hatukujaribu kulishughulikia na juhudi zinaendelea. Hata wakati huu ambapo nafikia ukingoni mwa kipindi changu cha uongozi, naendelea na nitaendelea kuyashughulikia mambo ya wafanyakazi mpaka nitakapokabidhi kijiti kwa kiongozi wetu mpya.

Ninawaomba tuendelee kushirikiana mpaka wakati huo na muendelee kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano kama mlivyofanya wakati wangu. Tena ningefurahi kuona ushirikiano wenu ukiwa mkubwa zaidi hata kuliko wakati wangu. Ni jambo lenye maslahi kwa pande zote: Serikali, wafanyakazi na nchi yetu.

Fursa za Ajira
Ndugu Wafanyakazi;
Serikali imeendelea kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo la ajira nchini. Itakumbukwa kuwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2005 – 2010 Chama cha Mapinduzi kiliahidi ajira mpya milioni moja. Tulifanikiwa kuzalisha ajira milioni 1,271,923 ambazo ni zaidi ya lengo. Katika kipindi cha miaka mitano hii, tayari tumeshazalisha ajira milioni 1,381,621. Na hivyo kufikisha jumla ya ajira milioni 2,653,544 katika kipindi cha miaka 10. Kati ya hizo ajira 600,547 zilitokana na sekta ya umma na ajira milioni 2,052,997 zimetokana na sekta binafsi.

Pamoja na mafanikio hayo, bado tatizo la ukosefu wa ajira ni kubwa hapa nchini na hasa miongoni mwa vijana. Hivyo basi, tutaendelea na tunaendelea na utekelezaji wa mikakati na mipango ya kukuza ajira nchini. Wizara ya Kazi na Ajira ikishirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, imefanya utafiti wa nguvu kazi nchini tangu mwezi Februari, 2014 ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Mei, 2015. Utafiti huu utatoa taarifa za soko la ajira nchini ikijumuisha hali halisi ya kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana.

Napenda kurudia maneno niliyowahi kuyasema awali kuwa, kwa wakati wa sasa uwezo wa sekta ya umma kuajiri watu wengi si mkubwa na kwamba jawabu la ajira liko katika sekta binafsi. Azma ya Serikali ni kuendelea kujenga mazingira mazuri ya kurahisisha ukuaji wa sekta binafsi na kuvutia wawekezaji kuongeza mitaji ili kuongeza ajira. Tumefanya hivyo, na matokeo yake tumeyaona. Tutaendelea kufanya hivyo, sasa na siku zijazo.
Hitimisho

Ndugu Rais wa TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi;
Naomba nimalize hotuba yangu kwa kurudia kuwashukuru kwa dhati Wafanyakazi wote na viongozi wote wa vyama vya wafanyakazi nchini kwa ushirikiano mlionipa katika kipindi chote cha uongozi wangu. Kimsingi ushirikiano na ushauri wenu ulikuwa wa msaada mkubwa sana kwangu na wenzangu wote katika Serikali kuhusu namna iliyo bora ya kuzikabili changamoto mbalimbali za wafanyakazi nchini. Ushirikiano wetu huo ndio uliotuwezesha kwa pamoja kuzitafutia ufumbuzi. Najua kwamba hazikuisha zote. Nawaahidi kuwa Rais ajaye nitamkabidhi orodha ya yale ambayo bado ni kiporo. Ni imani yangu kwamba mtaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Awamu ya Tano itakayokuwapo baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2015.
Ndugu wafanyakazi;

Narudia kuwashukuru tena kwa kunialika kwenye sherehe za mwaka huu ambazo zinanipa nafasi ya kuagana nanyi kama Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania. Nawashukuru sana kwa wema wenu huo mlionifanyia. Nawatakia kila la heri katika kutimiza majukumu yenu ya ujenzi wa nchi yetu. Daima nitawakumbuka. Ninawapenda sana na nitaendelea kuwapenda.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!

Asanteni kwa kunisikiliza.