Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka leo jioni tarehe 6 Mei, 2014 kuelekea Abuja, Nigeria kuhudhuria Mkutano wa siku 3 wa Uchumi Duniani kuhusu Afrika (World Economic Forum).
Mkutano huo unaoanza kesho tarehe 7 – 9 Mei, 14, utahudhuriwa na viongozi kutoka Afrika na duniani kwa ujumla. Pamoja na mambo mengine mkutano utajadili njia mbalimbali zitakazolifanya Bara la Afrika kuumudu ukuaji wa kiuchumi kwa pamoja na fursa za ajira zinajitokeza.
Katika Mkutano huo, viongozi pia watajadiliana jinsi ya kugharamia miundo mbinu Barani Afrika, njia za kukuza biashara baina ya nchi zao na uwekezaji katika sekta ya kilimo barani
Chini ya kaulimbiu ya “Forging Inclusive Growth, Creating Jobs” viongozi pia watajadili kwa pamoja namna ya kukuza uchumi na uwekezaji kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Wakiwa Abuja viongozi pia watapata nafasi ya kujadili changamoto zinazolikabili Bara la Afrika zikiwemo za ukosefu wa ajira, matishio ya kiusalama, vikwazo vya usafiri barani , upungufu wa chakula na athari kadhaa za mazingira .
Akiwa mjini Abuja Rais Kikwete atakutana na viongozi kadhaa wa Afrika na Dunia kwa ujumla ambao wapo Abuja wakiwemo Waziri Mkuu wa China Bw. Li Keqian , Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu Bw. Gordon Brown ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza na viongozi kadhaa wa mashirika ya kiserikali na kibinafsi.