Jumanne , 11th Oct , 2022

Kigodi Juma (24), mkazi wa Kijiji cha Nkiniziwa kilichopo wilaya ya Nzega mkoani Tabora, amejuruhiwa vibaya katika maeneo ya mwili wake baada ya kupigwa na shoti ya umeme wakati akikata nguzo ya umeme kwa kutumia shoka, majira ya usiku.

Kigodi Juma, aliyepigwa shoti ya umeme

Akitoa ufafanuzi  wa tukio hilo  Afisa Mtendaji wa Kata ya Nkiniziwa Hamisi Bundu, amesema kijana huyo alitenda tukio hilo usiku wa kuamkia Oktoba 10, 2022 ambapo majira  hayo ya usiku walishtushwa na kukatika kwa huduma ya umeme.

Amesema kijana huyo kabla ya kuanza kukata nguzo hiyo alirusha waya uliokuwa umefungwa vipande vya miti kwa ajili ya kupigisha shoti  ili umeme uweze kukatika ili apate urahisi wa kuangusha nguzo hiyo bila wasiwasi wa kujeruhiwa na umeme  pasipo kujua kama umeme bado ulikuwa haujakatika.

Kijana huyo baada ya kupigwa shoti ya umeme alikimbizwa katika kituo cha afya  Busondo na kwa sasa anaendelea na matibabu, huku Kaimu Mganga wa kituo hicho cha afya  Juma Sosoma, akieleza licha ahueni aliyonayo kwa sasa ataandikiwa rufaa ya kwenda  katika  hospitali kubwa kwa ajili ya vipimo  zaidi  vya  ndani ya mwili kutokana na kuumia vibaya  katika maeneo ya miguu,shingo ,usoni  na kwenye mikono.