Javier Pérez de Cuéllar
Katibu Mkuu huyo wa tano ameacha mchango wa amani duniani kote kutokana na juhudi zake za kuimarisha mazungumzo, kuleta pande kinzani pamoja na kufanikisha usuluhishi.
Katibu Mkuu huyu wa kwanza wa UN kutoka nchi za Amerika ya Kusini alishikilia maadili ya Umoja wa Mataifa hata baada ya kumaliza kipindi chake cha uongozi, akichechemua amani, haki, haki za binadamu na utu wa binadamu wakati wote wa uhai wake.
Alizaliwa Lima, Peru mwaka 1920 ambapo alishika wadhifa wa juu kabisa katika Umoja wa Mataifa baada ya kuwa mwanadiplomasia wa nchi yake kwa miaka 40. Mwaka 1946 akiwa mwanadiplomasia kijana, alishiriki kwenye mkutano wa kwanza wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Kabla ya kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu alikuwa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Cyprus halafu akawa msadizi wa Katibu Mkuu wa UN wa masuala maalum ya Siasa.
Katibu Mkuu Peres De Cuellar alishiriki majadiliano ya kisiasa duniani kote. Aliongoza mashauriano baina ya Uingereza na Argentina kwenye mzozo kati yao juu ya visiwa vya Falklands au Malvinas.
Alikuwa msuluhishi kwenye sitisho la mapigano mwaka 1988 lililomaliza vita kati ya Iran na Iraq. Alisaidia kuondoa majeshi ya Urusi kutoka Afghanistan. Timu yake iliandaa mpango wa Amerika ya Kati, Uliowezesha Umoja wa Mataifa kufuatilia uchaguzi wa Nicaragua.
Alisaidia kukamilika kwa uchaguzi wa serikali mpya ya Cambodia uliokuwa umegubikw na vikwazo lukuki.
Hali kadhalika alisaidia kipindi cha mpito cha kuelekea Uhuru wa Namibia. Na siku yake ya mwisho ofisini alikamilisha makubaliano ya amani Elsavador.
Javier Peres De Cueller alisema amani ni lazima iwe ushindi kwa wote bila kuwepo kwa walioshindwa.
