Jumamosi , 21st Jun , 2014

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ni mzuri, umeleta matumaini kwa kupanua wigo na kufungua zaidi uwanja wa kisiasa pamoja na kuiwajibisha Serikali.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ni mzuri, umeleta matumaini kwa kupanua wigo na kufungua zaidi uwanja wa kisiasa pamoja na kuiwajibisha Serikali.

Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa ili mfumo huo uboreshwe zaidi na uweze kuimarisha misingi mikuu ya maendeleo ni lazima uendeshwe kwa watu kufuata sheria na wala siyo kuingiza matumizi ya nguvu ambayo yanaweza kuvuruga nchi.

Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama aliyasema hayo jana Ijumaa, Juni 20, 2014, wakati alipotoa Mhadhara (Lecture) kuhusu Usalama wa taifa – The Security of a Nation- kwenye Chuo cha Taifa cha Ulinzi - National Defence College (NDC) Kunduchi, mjini Dar es Salaam.

Rais Kikwete alikuwa anajibu swali la mwanafunzi wa kozi ya pili kwenye chuo hicho kutoka Kenya ambaye alitaka kujua jinsi gani vyama vingi vya siasa vinavyoathiri umoja wa kitaifa na kuibadilishaTanzania kufuatia miaka zaidi ya 30 ya Tanzania kuwa nchi yenye kuleta matumaini kwa nchi nyingine za Afrika na Waafrika.

Rais kikwete alisema: “Vyama vingi ni vizuri. Mfumo wa vyama vingi unaleta matumaini kwa kupanua wigo wa kisiasa ambao haukuwa mpana kiasi hicho huko nyuma. Sasa mtu anaweza kuamua kujiunga na chama chochote cha siasa anachokipenda yeye.”
Aliongeza rais Kikwete: “Ni mfumo ambao unaiwajibisha Serikali. Ni mfumo mzuri kwa upanuzi wa demokrasia. Sasa watu wanaweza hata kuamua kupunguza bajeti ya safari za Rais nje ya nchi. Wanadhani kuwa Rais anaweza kufanikiwa zaidi na Tanzania kupita hatua za maendeleo haraka zaidi kama Rais atabakia amejifungia ndani ya nchi.”

Rais Kikwete alizidi kujibu swali hilo: “Jambo la maana ni kwamba tunahitaji aina mbali mbali za mawazo. Mawazo ya namna hiyo hayaathiri demokrasia. Mawazo ya namna hiyo yanasaidia hata chama changu kuimarika zaidi.”

Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa mfumo huo utavurugika endapo baadhi ya watu wataendekeza matumizi ya nguvu na hoja za nguvu badala ya kupambana kwa hoja na nguvu ya hoja.

“Wasiwasi wangu ni kuingiza matumizi ya nguvu katika ujenzi wa demokrasia. Ni makosa kwa watu kukimbilia kutumia nguvu baada ya kushindwa kwenye hoja. Na hili halivumiliki na likitokea basi Serikali itaingilia kati kudumisha amani.”