Utumishi wa Umma nchini kubadilika katika utendaji wao ili kuwa wawezeshaji zaidi badala ya wakwamishaji katika kutoa maamuzi yanayopelekea utendaji wa shughuli mbalimbali nchini.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo leo wakati akifungua Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 10 ya Tume ya Utumishi wa Umma jijini Dar es Salaam.
“Watu wanaona utumishi wa Umma kama wakwamishaji wa maamuzi, jitazameni, Utumishi wa Umma unaelezewa kama wakwamishaji badala ya kuwa wawezeshaji, mkiendelea kuwa hivyo mtachelewesha sana maendeleo.” Rais amesema na kueleza kuwa katika mazingira tuliyonayo na tunayoyaendea, mtazamo wa kuzuia na kuchelewesha shughuli za wananchi hauna tija wala manufaa kwa Taifa.
“Lazima mbadilishe mtazamo wa utumishi wa Umma uwe wa kibiashara na wa kufanya maamuzi kwa haraka, kwa makini na kwa weledi zaidi ili kujenge imani kwa wananchi na wawekezaji ambao wanakuja nchini” .
Rais amewaasa na kuongeza kuwa Utumishi wa Umma unatarajiwa kuendelea kusimamia na kutenda haki tena kwa wakati, kwani haki inayocheleweshwa ni haki inayopokonywa.
Rais amesema wakati Tanzania inatazamiwa kufikia nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, Utumishi wa Umma unatakiwa kuwa imara na unaoweza kufikisha nchi kwenye lengo hilo la Maendeleo la Taifa (Tanzania Development Vision 2025).
“Tume inapaswa kujipanga vyema ili kuwawezesha watumishi wake kutimiza wajibu wake na kuendelea kuhimiza na kusimamia nidhamu, weledi na uadilifu”. Rais amesema na kuongeza kuwa Wananchi, Tume ya Marekebisho ya katiba na Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wameona umuhimu wa Tume ya Utumishi wa Umma na sasa jambo hilo liko kwenye Katiba Inayopendekezwa.