
Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha
Akitoa taarifa hiyo leo, Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha ACP Charles Mkumbo amesema katika tukio la kwanza jana saa 4:00 usiku katika kijiji cha Kimbolo wilayani Arumeru, watu watano wote wakazi wa kijiji cha Kyoga walifariki dunia baada ya gari aina ya Toyota Premio lenye namba za usajili T 579 BSG kusombwa na maji.
Amewataja watu hao waliofariki katika tukio hilo kuwa ni Shengai Saiguran (30), Nembris Mungaya (20), Minis Loyi (25), Inoti George (40) na Ngaisi Moluo ambaye umri wake bado haujafahamika mara moja huku dereva wa gari hilo Yusuph Jacobo akinusurika.
Kamanda Mkumbo amesema mbali na vifo vya watu hao pia watu wengine wawili walifariki dunia katika maeneo tofauti ambapo katika kijiji cha Keriani mtu aitwaye Babu Robikeki alisombwa na maji kisha kufariki dunia wakati anavuka mto wakati akitokea matembezini.
Mtu wa katika matukio hayo ni Seuli Meseyeki (37) dereva wa bodaboda ambaye alikuwa anaendesha pikipiki aina ya T-Better yenye namba za usajili T. 726 DFD ambaye alisombwa na maji eneo la Olorieni Ngaramtoni wakati anavuka barabara.
Kamanda Mkumbo pia amesema pikipiki aina ya Boxer yenye namba za usajili MC 892 ACR iliokotwa maeneo ya Olasiti kwa Mawala halmashauri ya jiji la Arusha huku dereva wake hajulikani alipo.