Jumatano , 4th Nov , 2020

Mchakato wa kuigawa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuwa na Manispaa zaidi ya moja umekamilika baada ya viongozi kuanza utaratibu.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ameyasema  hayo wakati wa kikao cha kujadili maendeleo ya Mkoa  ambacho kiliwahusisha  viongozi wa dini na taasisi mbalimbali, ambapo amesema tayari wataalam wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya wameandaa andiko la kuwasilisha kwenye vikao vyake vya madiwani mara baada ya kuapishwa.

Chalamila amesema  mchakato huo ni ahadi aliyoitoa Rais Mteule Dk. John Magufuli wakati wa kampeni za kuomba urais  mkoani humo ambapo alidai akipata ridhaa ya kiti hicho ataongeza manispaa ili kusongeza huduma za kijamii karibu na wananchi.

Hata hivyo Mwakilishi wa wabunge wateule wa Mkoa wa Mbeya, Anthon Mwantona kutoka Jimbo la Rungwe, amewahidi  wanambeya kuwa kazi kubwa watakayoifanya wabunge hao ni kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo yatachangia mkoa wa Mbeya kuwa wa mfano bila kujali itikadi za kisiasa.