Jumanne , 15th Dec , 2015

Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan nchini Mhe. Masaharu Yoshida Ikulu jijini Dar es salaam, ambapo Balozi huyo amempongeza Dkt. Magufuli kwa kuchaguliwa kuingoza Tanzania katika awamu ya tano.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Balozi wa Japan nchini Masaharu Yoshida aliyefika Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo.

Pamoja na pongezi hizo viongozi hao wamezungumzia uhusiano mzuri uliopo kati ya Japan na Tanzania ambapo Balozi Yoshida amemhakikishia Rais Magufuli kuwa Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo

Baadhi ya miradi ya maendeleo waliyozungumzia ni ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi namba mbili utakaozalisha megawatts 240 za umeme na utakaogharimu Dola za kimarekani milioni 344.2 kwa ufadhili kutoka Japan na Mradi wa ujenzi wa barabara ya Mwenge hadi Bagamoyo awamu ya pili.

Miradi mingine ni ujenzi wa Barabara ya Gerezani - Bendera tatu Jijini Dar es salaam na ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya TAZARA ambayo taratibu za kuanza kwa ujenzi tayari zimeanza baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa ujenzi mwezi Oktoba mwaka huu

Aidha Balozi Yoshida amemuarifu Rais Magufuli juu ya ujio wa Mjumbe maalumu kutoka Japan Mheshimiwa Seiji Kihara anayetarajiwa kuwasili kesho hapa nchini kwa madhumuni ya kuwasilisha ujumbe maalumu kutoka kwa Waziri Mkuu wa Japan Mheshimiwa Shinzo Abe.