Jumanne , 13th Mei , 2014

Kumekuwa na Idadi ndogo ya wanafunzi waliohitimu kidato cha sita nchini Tanzania wanaojiunga na mafunzo ya Taifa Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria kutokana na wanafunzi wengi kuanza masomo mwezi Oktoba katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu.

Baadhi ya wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwa katika mafunzo ya Hiari na ya uzalendo katika moja ya kambi za jeshi la kujenga taifa JKT.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa JKT, Dkt. Hussein Mwinyi wakati akitoa makadirio ya Bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2014/2015 ambapo katika awamu ya tatu ya mafunzo hayo wamejiunga vijana 1,002 kati ya 15,000 waliokusudiwa huku awamu ya nne ikikosa wanafunzi waliojiunga.

Kwa Upande mwingine, Dkt. Mwinyi amesema serikali itaendelea kuwalipa fidia wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania( JWTZ) kwa ajili ya matumizi ya kijeshi huku baadhi ya maeneo wakiwa tayari wameshalipwa.