Jumapili , 12th Oct , 2025

Kinyang'anyiro kati ya wagombea wawili wakuu katika uchaguzi wa Ushelisheli kiliamuliwa katika duru ya pili baada ya kukosekana mshindi wa moja kwa moja katika kura ya urais wiki mbili zilizopita.

Kiongozi wa upinzani nchini Ushelisheli, Patrick Herminie ameshinda uchaguzi wa urais na kumshinda kiongozi aliye madarakani Wavel Ramkalawan katika kura ya marudio, kulingana na matokeo rasmi yaliyotolewa mapema leo Jumapili.

Herminie amepata 52.7% ya kura, huku Ramkalawan akipata 47.3%. Herminie ambaye alihudumu kama spika wa bunge la kitaifa kati ya 2007 na 2016 anawakilisha chama cha United Seychelles, ambacho kiliongoza nchi hiyo kwa miongo minne kabla ya kupoteza mamlaka mwaka wa 2020. Kilikuwa chama tawala kutoka 1977 hadi 2020. Ramkalawan kwa upande wake, wa chama tawala cha Linyon Demokratik Seselwa, alikuwa akitafuta muhula wa pili.

Kinyang'anyiro kati ya wagombea wawili wakuu katika uchaguzi wa Ushelisheli kiliamuliwa katika duru ya pili baada ya kukosekana mshindi wa moja kwa moja katika kura ya urais wiki mbili zilizopita. Upigaji kura wa mapema ulianza Alhamisi, lakini watu wengi katika taifa hilo katika visiwa hivyo vya Bahari ya Hindi walipiga kura jana Jumamosi.

Wote wawili, Herminie na Ramkalawan wakiendesha kampeni wliahidi kushughulikia masuala muhimu, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira na mgogoro wa uraibu wa dawa za kulevya katika nchi hiyo ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikionekana kama kimbilio la watalii.

Wiki moja kabla ya duru ya kwanza ya upigaji kura, wanaharakati waliishtaki serikali, wakipinga uamuzi wa hivi karibuni wa kutoa ukodishaji wa muda mrefu wa eneo la mita za mraba 400,000 (ekari 100) kwenye kisiwa cha Assomption, moja ya visiwa 115 nchini humo, kwa kampuni ya Qatar ili kuendeleza hoteli ya kifahari.

Nchi hiyo imekuwa na mazingira mazuri ya uchumi unaotokana na utalii, ambao umeifanya kuwa kileleni mwa orodha ya nchi tajiri zaidi barani Afrika kwa pato la taifa kwa kila mtu, kulingana na Benki ya Dunia.