Mwenyekiti wa chama hicho, Farooq Ahmed, amesema kuna uvumi uliosambaa nchini kwamba kutakuwa na mgomo wa wenye vituo kupinga kushuka kwa bei hali iliyosababisha taharuki kwa wananchi.
Amesema kilichotokea ni ucheleweshaji wa mafuta katika vituo vichache kwenye maeneo kadhaa kulikotokana na mpangilio baada ya kupangwa kwa bei mpya lakini hakuna mgomo wowote uliopangwa na mafuta yanapatikana kwa wingi.
Amesema vituo vyote vya mafuta vinaendelea na vitaendelea kuuza mafuta kama kawaida na kwa bei iliyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) na kwamba hakuna sababu ya kuhofia.
Farook amesema taharuki hiyo ilisababisha wananchi wengi kukimbilia kwenye vituo vya mafuta na kujaza mafuta mengi huku wengine wakienda na madumu kwa ajili ya kuweka akiba.
“Huo ni uvumi tu na hakuna kitu kama hicho hivyo watanzania waendelee kuweka mafuta kama kawaida wasiweke akiba kwa kuwa mafuta yatakuwepo na hakutakuwa na mgomo wowote,” alisema mwenyekiti huyo.